• HABARI MPYA

  Sunday, May 15, 2016

  PLUIJM AWAACHA WANNE SAFARI YA ANGOLA, ABEBA ‘KIKOSI KAZI’

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amewaacha wachezaji wanne katika safari ya Angola asubuhi ya kesho kwa sababu mbalimbali.
  Hao ni kipa Benedicto Tinocco ambaye hayumo kwenye programu za mchezo sawa na viungo Said Juma na Issoufou Boubacar, wakati Malimi Busungu ni majeruhi. 
  Yanga inatarajiwa kuondoka Saa 12:00 asubuhi ya kesho kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Sagrada Esperanca Jumatano.
  Katika mchezo huo, Yanga itahitaji hata sare kusonga mbele, baada ya awali kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony.
  Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm (kulia) akiwa na Waziri wa Kilimo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba
  Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
  Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
  Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
  Kila la heri na safari njema Yanga SC.

  KIKOSI CHA YANGA KINACHOKWENDA ANGOLA;
  Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
  Mabeki; Juma Abdul, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
  Viungo; Thabani Kamusoko, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
  Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony, Amissi Tambwe na Paul Nonga.
  BENCHI LA UFUNDI;
  Kocha Mkuu; Hans van der Pluijm (Uholanzi)
  Kocha Msaidizi; Juma Mwambusi
  Kocha wa makipa; Juma Pondamali
  Daktari; Edward Bavu
  Mchua Misuli; Jacob Onyango
  Mtunza Vifaa; Mohammed Mpogolo
  Meneja; Hafidh Saleh
  WACHEZAJI WALIOBAKI DAR;
  Benedicto Tinocco, Said Juma, Issoufou Boubacar na Malimi Busungu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PLUIJM AWAACHA WANNE SAFARI YA ANGOLA, ABEBA ‘KIKOSI KAZI’ Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top