• HABARI MPYA

  Saturday, May 14, 2016

  NDANDA YAIKATALIA YANGA SHEREHE ZA UBINGWA, SARE 2-2 TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga ambao tayari ni mabingwa wa Ligi Kuu, kwa sare hiyo wanafikisha pointi 72 baada ya kucheza mechi 29 na watacheza mechi yao ya mwisho na Majimaji mjini Songea wiki ijayo.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Selemani Kimigani wa Morogoro, aliyesaidiwa na washika vibendera Kudra Omary wa Tanga na Abdallah Rashid wa Pwani, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
  Wafungaji wa mabao ya Yanga, Donald Ngoma (kushoto) na Simon Msuva (kulia) wakipongezana
  Kiungo wa Ndanda, Kiggy Makassy akiupitia mpira miguuni mwa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima

  Ndanda ndiyo waliotangulia kupata bao kwa penalti dakika ya 29, mfungaji Omary Mponda aliyemchambua vizuri kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ baada ya beki Juma Abdul kumuangusha mshambuliaji Atupele Green kwenye boksi.
  Yanga walisawazisha bao hilo dakika ya 36 kupitia kwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Simon Msuva kwa shuti kali akimalizia krosi ya winga Geoffrey Mwashiuya.
  Mshambuliaji hatari kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 41 kwa shuti kali pia akimalizia krosi ya beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali.  
  Kipindi cha pili, timu zote zilianza na mabadiliko, Yanga wakimpumzisha Mwinyi Mngwali na kumuingiza Oscar Joshua na Ndanda wakimpumzisha Riffat Hamisi na kuingia Ahmed Msumi.
  Mabadiliko hayo yaliinufaisha Ndanda iliyopata bao la kusawazisha dakika ya 79 lililofungwa na Minely aliyemalizia pasi ya Atupele Green.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali/Oscar Joshua dk46, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Mbuyu Twite dk85, Amissi Tambwe, Donald Ngoma/Matheo Anthony dk74, Geoffrey Mwashiuya.
  Simba SC; Jackson Chove, Aziz Sibo, Cassian Ponera, Riffat Hamisi/Ahmed Msumi dk46, Hemed Khoja, William Lucian, Kiggi Makassy, Bryson Raphael, Omary Mponda, Atupele Green na Burhan Rashid/Salum Minely dk40. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDANDA YAIKATALIA YANGA SHEREHE ZA UBINGWA, SARE 2-2 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top