• HABARI MPYA

    Saturday, May 14, 2016

    NAFASI YA PILI LIGI KUU YAGEUKA ‘DILI’ TENA, NI SIMBA AU AZAM?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa timu zote 16 kuingia viwanjani.
    Leo kutakuwa na mchezo mmoja wenye hadhi ya kuhitimisha msimu wa 2015/2016 kati ya mabingwa, Yanga SC na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ndanda ndiyo wenyeji wa mchezo wa leo ingawa watacheza nyumbani kwa Yanga, baada ya makubaliano ya timu hizo yaliyopewa baraka na Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Yanga iliipigia magoti Ndanda kuomba mchezo huo uchezwe Dar es Salaam badala ya Nangwanda Sijaona, Mtwara kwa sababu wanaondoka kesho Alfajiri kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Jumanne.
    Na ‘waungwana’ Ndanda wakaikubalia ombi hilo Yanga na sasa mchezo huo unachezwa Dar es Salaam.
    Mchezo wa leo hauna faida zaidi kwa timu zote, kwani Yanga tayari bingwa na Ndanda FC imekwishajihakikishia kuendelea kuwa memba wa Ligi Kuu msimu ujao.
    Mchezo wa leo utakwenda sambamba na sherehe za kukabidhi Kombe kwa mabingwa, Yanga SC na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.    
    Simba SC inawania tena nafasi ya pili Ligi Kuu

    MECHI ZA KESHO;
    Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tano kwenye viwanja tofauti.
    Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wenyeji Mtibwa Sugar wataikaribisha Simba SC, Uwanja wa Kambarage Shinyanga wahamiaji, Kagera Sugar ya Bukoba watamenyana na wenye mji wao, Stand United na Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Mbeya City.
    Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Prisons wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza na Uwanja wa MKwakwani, Tanga African Sports watakuwa wenyeji wa Azam FC.
    Pazia la Ligi Kuu litafungwa rasmi Mei 21, 2016 kwa mechi saba, Mbeya City Vs Ndanda FC (Mbeya), Coastal Union Vs Prisons (Tanga), Simba SC Vs JKT Ruvu (Dar es Salaam), Toto Africans Vs Stand United (Mwanza), Azam FC Vs Mgambo JKT (Dar es Salaam), Kagera Sugar Vs Mwadui FC (Shinyanga), Mtibwa Sugar Vs African Sports (Morogoro) na Majimaji Vs Yanga SC (Ruvuma).
    Azam FC inawania kumaliza katika katika nafasi ya pili

    NAFASI YA PILI;
    Wakati Yanga SC imekwishajihakikishia ubingwa baada ya kufikisha pointi 71 kutokana na mechi 28, vita ya kuwania nafasi ya pili bado ipo kwa Azam FC na Simba.
    Azam FC kwa sasa inashika nafasi ya pili kwa pointi zake 60 na Simba SC ni ya tatu kwa pointi zake 59, zote zikiwa zimecheza mechi 28.
    Azam FC wanamenyana na Sports kesho ambayo inapigana kuepuka kushuka daraja, wakati Simba inamenyana na Mtibwa ambayo haina cha kupigania.
    Katika mechi za mwisho, Azam itamaliza na Mgambo JKT na Simba itamaliza na JKT Ruvu. Zote JKT Ruvu na Mgambo zinapambana kuepuka kushuka daraja.
    Hiyo inamaanisha vita ya nafasi ya pili bado ngumu.
    Yanga SC tayati ni mabingwa tena wa Ligi Kuu

    KWA NINI NAFASI YA PILI NI DILI TENA
    Mwanzoni mwa msimu nafasi ya pili katika Ligi Kuu ilipoteza heshima kufuatia kurejea kwa michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambayo sasa inatoa timu ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
    Lakini baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuongeza idadi ya timu za kuingia hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kutoka nane za makundi mawili hadi 16 za makundi manne kuanzia mwaka ujao, nafasi ya pili ni dili tena.
    Hiyo inatokana na matumaini ya Tanzania kuongezewa nafasi ya kuingiza timu kwa hatua za awali za michuano ya Afrika kutoka mbili za sasa, yaani moja moja kila michuano.
    Sasa Azam na Simba wanazipa tena uzito mechi zao za kumalizia ligi ili kuwania nafasi ya pili.
    African Sports ipo kwenye hatari ya kuungana na Coastal Union kushuka daraja?

    ZA KUPUNGIA MKONO WA KWAHERI LIGI KUU
    Coastal Union ni kama tayari imekwishashuka, lakini Toto, JKT Ruvu, African Spors, Kagera Sugar na Mgambo JKT kati yao zinaweza kupatikana timu mbili nyingine za kuipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu.
    Toto inahitaji kushinda mchezo mmoja kati ya miwili iliyobaki ili kujihakikishia kubaki Ligi Kuu sawa na JKT Ruvu. Hali mbaya zaidi kwa Kagera Sugar, African Sports na Mgambo JKT.
    Sports ina pointi 26 za mechi 28, Kagera ina pointi 25 za mechi 28, Mgambo ina pointi 24 za mechi 28, wakati Coastal inayoshika mkia ina pointi 22 za mechi 29. Nani atanusurika?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NAFASI YA PILI LIGI KUU YAGEUKA ‘DILI’ TENA, NI SIMBA AU AZAM? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top