• HABARI MPYA

    Wednesday, May 18, 2016

    NA HAWA WA INDIA, AU KAMA WALE WA BRAZIL NA AFRIKA KUSINI?

    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania, Serengeti Boys jana ilishinda mechi ya kwanza katika michuano ya kirafiki ya vijana Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa, India.
    Serengeti Boys iliwafunga wenyeji, india mabao 3-1 na kufikisha pointi nne katika michuano hiyo.
    Mabao ya Serengeti Boys jana yalifungwa na Amani Maziku dakika ya 20 na 28 na Asad Ali dakika ya 47, wakati la india lilifungwa na Komal Thatal dakika ya 36.
    Katika Mchezo wake wa kwanza, Serengeti Boys ilitoa ya sare kufungana bao 1-1 na Marekani.
    Kwa ushindi huo, Serengeti Boys sasa watahitaji angalau sare au ushindi wa mchezo mmoja kati ya miwili waliyobakiza, dhidi ya Korea Kusini kesho na Malaysia Jumamosi, ili kutinga Nusu Fainali ya michuano hiyo iliyoanza Mei 12 na inatarajiwa kufikia tamati Mei 26, mwaka huu.

    Michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka India (AIFF) ili kuipa mazoezi timu yake kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana mwaka 2017 ambazo watakuwa wenyeji.
    Matokeo hayo yamepokewa vizuri na Watanzania na kwa ujumla wamewafurahia vijana hao.
    Mapendekezo mengi kwa TFF ni kuwashika na kuwaendeleza vijana hao, ili waje kuunda timu bora ya taifa baadaye.
    Ni ushauri mzuri na unaokuja katika wakati mwafaka, kwani tayari Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amekwishaweka wazi dhamira yake juu ya soka ya vijana.
    Mara tu baada ya kuingia ofisini pale Uwanja wa Karume, jambo la kwanza kulitilia mkazo Malinzi lilikuwa ni soka ya vijana.
    Na akafanikiwa kuishawishi CAF (Shirikisho la Soka Afrika) kuipa Tanzania uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika ya vijana umri chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.
    Hakika hiyo ilikuwa ni hatua nzuri kwa Tanzania katika kujenga msingi imara wa soka ya vijana – kwani kwa kuwa mwenyeji Serengeti Bosy itacheza fainali za kwanza za U-17 kihistoria. 
    Na katika kuandaa kikosi bora cha kushiriki fainali hizo, Juni mwaka jana TFF ilifanya mashindano ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 13 mjini Mwanza na kuteua wachezaji ambao sasa wanaandaliwa kwa ajili ya fainali za mwaka 2019.
    Lakini wakati programu hiyo, ikiendelea ikaundwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka jana, ambao kwa wakati wote imekuwa ikicheza mechi za kijipima nguvu kila mwishoni mwa mwezi.
    Timu hiyo ndiyo ambayo sasa ipo India na inajiandaa na mechi za kufuzu kwa fainali za U-17 mwakani, ikiwa imepangiwa kuanza na Shelisheli.
    Malinzi ameweza kutekeleza vizuri programu ya vijana hadi sasa – kwanza kwa kuhakikisha pamoja na changamoto zote timu inakutana kwa kambi kila mwisho wa mwezi na kucheza mechi.
    Na kabla ya India, timu hiyo ilicheza mechi mbili za kimataifa za kujipima nguvu dhidi ya Misri mjini Dar es Salaam miezi miwili iliyopita ikitoa sare moja na kushinda moja.
    Inaonekana wazi kwa sasa Serengeti Boys haiandaliwi kushiriki, bali inaandaliwa kushindana na malengo yapo.
    Ni tofauti kidogo na miaka ya nyuma, vijana walikuwa wanakusanywa ili kushiriki kwa kutimiza wajibu, lakini hakukuwa na dalili zozote za malengo.
    Wasiwasi uliopo kwa sasa ni mmoja tu, iwapo Serengeti Boys ya sasa haitafuzu kwenye fainali zijazo za U-17 vijana hawa wanaweza kutekelezwa kama ilivyokuwa kwa chipukizi wazuri waliowatangulia.
    Kwa nini wasiwasi huo? Kama hawatafuzu fainali za U-17 mwakani wanaweza kuchukuliwa hawatakuwa na faida tena, kwa sababu fainali za 2019 wapo vijana tayari wanaandaliwa.
    Watanzania wanakumbuka wale vijana walioshinda mashindano ya Copa Coca Cola Brazil na Afrika Kusini mara mbili mfululizo mwaka 2007 na 2008 walitekelezwa baadaye.
    Kwa miaka mingi, TFF imekuwa na mipango mizuri ya kuibua vipaji vya vijana, lakini tatizo linakuja katika kuwaendeleza kutoka umri wa Serengeti Boys hadi kuwa wachezaji wakubwa.
    Tunaacha vipaji vingi hapa katikati kwa kutokuwa tu na mkakati wa kuwaendeleza vijana.
    Kama kweli tunataka kukuza soka yetu nasi siku moja tuje kuwa na wachezaji wengi wakubwa na timu bora za taifa, lazima tufikirie namna ya kuwaendeleza vijana kutoka kwenye umri wa ujana hadi kuwa wachezaji wakubwa.
    Leo Maziku anaonyesha kipaji cha kufunga katika umri mdogo tu wa miaka 15 – je mkakati upi umeandaliwa kuhakikisha anaendeleza makali yake na kukua vizuri kisoka?
    Au ndiyo itakuwa kama wale chipukizi waliofanya vizuri Brazil na Afrika Kusini kwenye Copa Cola baadaye wakapotelea kusikojulikana? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NA HAWA WA INDIA, AU KAMA WALE WA BRAZIL NA AFRIKA KUSINI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top