• HABARI MPYA

  Sunday, May 08, 2016

  MSUVA AFIKISHA MECHI 150 YANGA AKIFUNGA BAO LA 47

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  WINGA wa Yanga, Simon Happygod Msuva (pichani kulia) jana amecheza mechi yake ya 150 katika timu hiyo na kufunga bao la 47 katika mashindano yote.
  Msuva alifunga bao la kwanza dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola dakika ya 72, Yanga ikishinda 2-0 katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania tiketi ya kuingia kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho. 
  Msuva alikuwa mwenye furaha baada ya mchezo wa jana, ambao sasa unamfanya aingie kwenye orodha ya magwiji wa kukumbukwa Jangwani sawa na akina Edibily Lunyamila, Mrisho Ngassa na wengine.
  “Nimefurahi kucheza mechi yangu ya 150 hapa Yanga na kufunga bao muhimu katika mchezo huu hatimaye tumeibuka na ushindi wa 2-0, ambao unatuweka katika mazingira mazuri ya kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho,”alisema Msuva akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana.  
  Kisoka, Msuva alianza kama kipa wakati anasoma shule ya Msingi ya Lions ya Magomeni, kabla ya kuhamia kucheza ndani baada ya kujiunga na akademi ya Wakati Ujao.
  Akiwa hapo alifanya vizuri na kuchukuliwa timu ya Mkoa wa Kinondoni kucheza mashindano ya Vijana ya Copa Coca Cola mwaka 2009 na alishika nafasi ya pili kwa ufungaji bora.
  Simon Msuva akipiga krosi katika mechi yake ya 150 Yanga SC
  Simon Msuva akimtoka beki wa Sagrada Esperanca jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

  kwa mafanikio hayo, akachukuliwa na akademi ya Azam kuendelezwa kisoka, ambako aliendelea kung’ara baada ya kuibuka Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Uhai mwaka 2010.
  Kiu ya kutaka kuanza kucheza soka ya ushindani zaidi mapema, ilimfanya ahamie Moro United mwaka 2011 baada ya kuona Azam anachelewa kupandishwa kikosi cha kwanza.
  Na baada msimu mmoja tu, Msuva akachukuliwa na Yanga mwaka 2012 ambako jana amecheza mechi yake ya 150, akifunga bao la 47.
  Simon Msuva akikimbia kushangilia bao lake la 47 jana Yanga SC jana Uwanja wa Taifa
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSUVA AFIKISHA MECHI 150 YANGA AKIFUNGA BAO LA 47 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top