• HABARI MPYA

  Saturday, May 14, 2016

  MKURUGENZI MTENDAJI VODACOM NDANI YA PATI LA UBINGWA YANGA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MKURUGENZI Mtendaji wa kampuni ya Vodacom Tanzania, wadhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Ian Ferrao (pichani kushoto), anatarajiwa kuhudhuria mchezo wa jioni ya leo kati ya Ndanda FC na Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mchezo wa leo ndiyo unahitimisha msimu wa 2015/2016 kati ya mabingwa, Yanga SC na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ingawa pazia rasmi litafungwa wiki ijayo.
  Na Ferrao atakuwa sambamba na mgeni rasmi, Waziri wa Kilimo na Uvuvi, Mwigulu Mchemba katika kukabidhi aawadi kwa mabingwa, Yanga SC.
  Ndanda ndiyo wenyeji wa mchezo wa leo ingawa watacheza nyumbani kwa Yanga, baada ya makubaliano ya timu hizo yaliyopewa baraka na Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Yanga iliipigia magoti Ndanda kuomba mchezo huo uchezwe Dar es Salaam badala ya Nangwanda Sijaona, Mtwara kwa sababu wanaondoka kesho Alfajiri kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Jumanne.
  Na ‘waungwana’ Ndanda wakaikubalia ombi hilo Yanga na sasa mchezo huo unachezwa Dar es Salaam.
  Mchezo wa leo hauna faida zaidi kwa timu zote, kwani Yanga tayari bingwa na Ndanda FC imekwishajihakikishia kuendelea kuwa memba wa Ligi Kuu msimu ujao.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tano kwenye viwanja tofauti.
  Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wenyeji Mtibwa Sugar wataikaribisha Simba SC, Uwanja wa Kambarage Shinyanga wahamiaji, Kagera Sugar ya Bukoba watamenyana na wenye mji wao, Stand United na Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Mbeya City.
  Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Prisons wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza na Uwanja wa Mkwakwani, Tanga African Sports watakuwa wenyeji wa Azam FC.
  Pazia la Ligi Kuu litafungwa rasmi Mei 21, 2016 kwa mechi saba, Mbeya City Vs Ndanda FC (Mbeya), Coastal Union Vs Prisons (Tanga), Simba SC Vs JKT Ruvu (Dar es Salaam), Toto Africans Vs Stand United (Mwanza), Azam FC Vs Mgambo JKT (Dar es Salaam), Kagera Sugar Vs Mwadui FC (Shinyanga), Mtibwa Sugar Vs African Sports (Morogoro) na Majimaji Vs Yanga SC (Ruvuma).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKURUGENZI MTENDAJI VODACOM NDANI YA PATI LA UBINGWA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top