• HABARI MPYA

  Friday, May 13, 2016

  MBUYU TWITE NA BOSSOU WAAANZA MAZOEZI LEO YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  NYOTA wawili wa kigeni wa Yanga, Mbuyu Junior Twite wa DRC na Vincent Bossou wa Togo wanatarajiwa kuanza mazoezi leo Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam.
  Wawili hao walishindwa kumalizia mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City Jumanne baada ya kuumia na kutoka kipindi cha kwanza.
  Beki anayeweza kucheza nafasi ya kiungo pia, Twite alimpisha Salum Telela dakika ya nane tu, wakati beki wa kati Bossou alimpisha na Kevin Yondan dakika ya 29 akiwa tayari amekwishaifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 15.
  Vincent Bossou na Mbuyu Twite wanarudi kazini leo Yanga baada ya mapumziko ya siku mbili
  Wakati Twite alishitua mwenyewe goti alipokuwa anajikunja kupiga mpira, Bossou alipigwa kiwiko na mchezaji wa Mbeya City na kutokwa damu nyingi hivyo wote kushindwa kuendelea na mchezo ambao Yanga ilishinda 2-0.
  Na baada ya mapumziko ya siku mbili, wawili hao wanaanza mazoezi leo Kurasini kujiandaa na michezo miwili ijayo kuanzia kesho dhidi ya Ndanda FC wa Ligi Kuu na Jumatano dhidi ya Sagrada Esperanca nchini Angola katika Kombe la Shirikisho Afrika.
  Mchezo wa kesho ni maalum kwa Yanga kukabidhiwa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu, wakati wa Jumatano Angola ni wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Mchezo wa kwanza Yanga ilishinda 2-0 Dar es Salaam na katikati ya wiki ijayo itahitaji kulazimisha sare ili kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza na pia kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua hiyo katika michuano hiyo.
  Na hiyo itakuwa ni rekodi nyingine kwa Yanga baada ya mwaka 1998 kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika – ikifuatiwa na Simba SC mwaka 2003.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBUYU TWITE NA BOSSOU WAAANZA MAZOEZI LEO YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top