• HABARI MPYA

    Monday, May 02, 2016

    KUNA SEHEMU MSONDO NA SIKINDE WANAPIGWA CHENGA YA MWILI

    AWALI ya yote nichukue fursa hii kusema kuwa onyesho la juzi usiku la Sikinde na Msondo lililofanyika TCC Club Chang’ombe lilinivutia sana na niliburudika mpaka baaasi.
    Binafsi naamini hizi ndiyo bendi zenye nyimbo nyingi tamu kuliko bendi yoyote ile katika historia ya muziki wa dansi hapa Tanzania. Bendi hizi zina hazina ya nyimbo kali zisizochuja, nyimbo zilizojaa tungo zilizokwenda shule, bendi ambazo ndiyo zimekuwa chachu ya kuibuka kwa wasanii wengi wa dansi wanaofanya vizuri kwenye bendi nyingine kibao. Sikinde na Msondo ni ‘Simba na Yanga’ ya muziki wa dansi.

    Lakini kwa bahati mbaya sana, mashabiki wa bendi hizi wanapatikana zaidi manyumbani badala ya ukumbini na hapo ndipo yanapoibuka maajabu mawili ya Msondo na Sikinde.
    Maajabu ya kwanza ni kwamba licha ya hazina ya nyimbo nzuri, hazina ya wanamuziki ‘mafundi’ wenye kujua A,B,C ya muziki, hazina ya historia ya kipekee, lakini bado bendi hizo zinatumbuiza mbele ya mashabiki wasiozidi 250 kwenye maonyesho yao ya kila wiki tena ya kiingilio cha bei rahisi kama sio bure kabisa.
    Inashangaza sana, kwanini watu wakauke hivyo ukumbini? Jibu la haraka haraka utakalopewa ni media haitoi nafasi.Wala sibishi, ni kweli kabisa media zimeutupa muziki wa dansi, lakini ndiyo iwe sababu ya wanamuziki wa dansi kukubali kufa kikondoo bila kupambambana? 
    Mbona kuna nafasi kubwa sana kwenye mitandao ya kijamii? Hivi wanamuziki wanafahamu kuwa mitandao ya kijamii kama facebook, instagram, yutube, blogs, twitter na nyinginezo zinaweza kuinyanyua nyimbo hadi kumshawishi mtu wa radio na televisheni kuitumia kazi yako?
    Mimi naamini zaidi ya watu 300 waliohudhiria onyesho lile la Jumamosi wametokana na mijadala, mabishano na majigambo yaliyofanyika kwenye kurasa za facebook katika kuelekea kwa show hiyo.
    Maajabu ya pili ninayoyaona katika bendi za Msondo na Sikinde ni pale maonyesho yao maalum yanapojaza umati mkubwa watu kupindukia tena kwa kiingilio cha bei mbaya.
    Ukipiga kwa kiingilio cha bei chee mahudhurio kiduchu, onyesho maalum la kiingilio cha bei mbaya watu nyomi!! hapa ndipo Sikinde na Msondo wanapopigwa chenga ya mwili, kwanini? Kipo cha kujifunza hapo.
    Ni kwamba Sikinde na Msondo bado ni bendi zenye mashabiki wengi ila wanachohitaji mashabiki wao ni maonyesho maalum yenye hadhi ya kipekee, jikumbushe tamasha la Gurumo, miaka 50 ya Msondo, miaka 37 ya Sikinde yote yalishona watu vizuri.
    Inawezekana Msondo na Sikinde wanapiga kwenye kumbi ambazo hazifanani tena na mashabiki wao, kumbi ambazo hazina usalama mzuri wa mteja na mali yake, kumbi ambazo  hazina mandhari ya kuvutia wala huduma nzuri ya vyakula na vinywaji.
    Ukipima maonyesho ya Msondo yanayofanyika Leaders Club na TCC Club, ukiangalia hadhi ya watu wanaofika sehemu hizo mbili halafu ukalinganisha na pale Kinondoni Bar mtaa wa Togo jirani na kituo kidogo cha polisi cha Mtambani, utabaini namna fikra zangu juu ya ukumbi bora inavyoweza kuwa sababu ya kudidimiza bendi kongwe.
    Angalia namna onyesho la wakongwe wenzao wa Njenje pale Salender Bridge Club linavyonona watu wenye hadhi za kila namna halafu vuta picha itakuwa vipi Njenje wakihamia DDC Kariakoo kila Jumamosi. Ni wazi kuwa mahudhurio yao yatapungua sana.
    Msondo na Sikinde wanapaswa kuingia kwenye kipindi cha mpito cha kutathmini upya soko lao na mazingira wanayopiga muziki wao, wakiiwashia njaa feni na kukubali kupiga show za kuunga unga kwenye kumbi za barazani watazidi kudidimia. Ipo haja ya wao kujiongeza na kupandisha hadhi yao kwa makusudi, ifike wakati wajijengee uwezo wa kuandaa matamasha  makubwa wao wenyewe badala ya kuketi kitako na kusubiri mapromota.
    Ipo haja ya Sikinde na Msondo kupunguza maonyesho yao ya kila wiki na kubakiza machache ambayo wataweza kuyaongezea nguvu ya promosheni. 
    Msondo na Sikinde wajiwekee ratiba ya kufanya maonyesho kama ya juzi angalau mara tatu kwa mwaka ili kutunisha mifuko yao na kufidia pengo la kupunguza maonyesho yao ya kila wiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUNA SEHEMU MSONDO NA SIKINDE WANAPIGWA CHENGA YA MWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top