• HABARI MPYA

    Sunday, May 08, 2016

    KUFANYA VIBAYA AZAM FC, BENCHI LA UFUNDI HALIWEZI KUKWEPA LAWAMA

    BAADA ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Azam FC ilijipanga upya kwa kuanzia kubadilisha benchi la Ufundi.
    Kocha Mganda George ‘Best’ Nsimbe akaondolewa na kurejeshwa Muingereza, Stewart John Hall ambaye baadaye alileta Wasaidizi wawilil, Muingereza mwenzake Mark Philip  na Mromania Mario Mariana walioungana na maofisa wawili waliobaki, Dennis Kitambi na Iddi Abubakar kocha wa makipa.
    Ikumbukwe Nsimbe alianza kama Msaidizi wa Mcameroon, Joseph Marius Omog ambaye aliondolewa kabla ya msimu kumalizika kufuatia Azam kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2 na El Marreikh ya Sudan.
    Baada ya mabadiliko ya benchi la Ufundi, ukafuatia usajili wa kishindo, nyota wapya kama Allan Wanga kutoka El Merreikh, Racine Diouf kutoka Senegal, Jean Baptiste Mugiraneza kutoka APR ya Rwanda, Ramadhani Singano ‘Messi’ kutoka Simba na Ame Ali ‘Zungu’ kutoka Mtibwa Sugar wakisajiliwa.
    Pamoja na kuukosa ubingwa wa msimu wa 2014-2015, lakini Azam FC ilikuwa timu bora kwa maana ya timu na hata wachezaji mmoja mmoja.
    Nyota kama Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Serge Wawa, Aggrey Morris, Said Mourad, Gardiel Michael, Waziri Salum, Kipre Balou, Mudathir Yahya, Abdallah Kheri, Himid Mao, Frank Domayo, Farid Mussa, Didier Kavumbangu, John Bocco na Kipre Tchetche tayari walikuwa kikosini.
    Matarajio baada ya mabadiliko ya benchi la Ufundi na usajili wa kishindo yalikuwa makubwa na mazuri – na kwa bahati nzuri timu ikaanza kwa kushinda taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame Agosti mwaka jana Dar es Salaam.
    Pamoja na kuanza msimu mpya kwa kufungwa na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii kwa matuta, pamoja na hayo bado matarajio yalibaki kuwa makubwa.
    Wasiwasi ukaanza kujitokeza baada ya Azam FC kutolewa mapema katika michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mapema mwaka huu.
    Katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam ikatolewa katika hatua ya 16 Bora na Esperance ya Tunisia baada ya kuanzia hatua ya 32 Bora ambako iliitoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini.
    Na ikumbukwe Bidvest ilitumia kikosi cha wachezaji wa akiba kutokana na kutokuwa na malengo na michuano hiyo.
    Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, timu inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ulitekeleza kila ambacho benchi la Ufundi lilihitaji katika programu zake.
    Timu ikaenda Zambia kushiriki mashindnao maalum ya kirafiki, mwishoni mwa Januari ambako walibeba Kombe baada ya mechi tatu.
    Lakini wakati msimu unaelekea ukingoni, Azam FC inahitaji miujiza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuboronga katika mechi zake za mwishoni mwa msimu.
    Ubingwa upo wazi zaidi kwa Yanga na kwa bahati mbaya zaidi hata nafasi ya pili katika Ligi Kuu ipo wazi zaidi kwa Simba SC.
    Nafasi pekee kwa Azam FC kurejea kwenye michuano ya Afrika mwakani ni kupitia Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) ambako imefika fainali na itacheza na Yanga baadaye mwezi huu.
    Msimu huu, Azam ilikuwa na benchi pana la Ufundi pengine kuliko kipindi chote na pia ilikuwa ina kikosi kipana kilichosheheni nyota.  
    Kilichoonekana kuiathiri Azam FC mwishoni mwa msimu ni wachezaji waliotumika kwa muda mrefu kuchoka na kulazimishwa kuendelea kucheza.
    Kiwango cha Nahodha John Bocco siku za karibuni kabisa kimeonekana kuyumba iwe kwa kuchoka au, vyovyote – lakini bado aliendelea kulazimishwa kucheza.
    Na si Bocco tu, wachezaji wengine kadhaa walionekana kabisa kuchoka na bado wakaendelea kulazimishwa kucheza. Swali, kwanini wachezaji waliochoka walilazimishwa kuendelea kucheza wakati timu ina kikosi kipana?
    Huwezi kumuambia mtu eti Allan Wanga si mchezaji mzuri ndiyo maana hakufanikiwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC chini ya Stewart hata Bocco akawa analazimishwa kucheza akiwa amechoka.
    Ame Ali aliivutia Azam FC kwa mabao yake aliyokua anafunga alipokuwa Mtibwa Sugar – lakini mbele ya Stewart hakuonekana kama mshambuliaji wa maana na akawa anayumbishwa, wakati mwingine akipangwa kama kiungo.
    Kavumbangu ghafla akaanza kuwekwa benchi akiwa katika kiwango kizuri hadi akapoteza hali ya kujiamini na hata benchi la Ufundi lilipolazimika kuanza kumtumia, tayari alikuwa amekwishaathirika kisaikolojia.
    Azam haijamaliza msimu, kwani ina mechi tatu za Ligi Kuu kuanzia leo na baadaye itakuwa na fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Yanga na sijui benchi la Ufundi la timu hiyo limegundua nini tatizo.
    Wakati tunasubiri kuona Stewart na benchi lake watamalizia vipi msimu Azam FC, lakini hadi sasa hawawezi kukwepa lawama za matokeo mabaya ya timu msimu huu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUFANYA VIBAYA AZAM FC, BENCHI LA UFUNDI HALIWEZI KUKWEPA LAWAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top