• HABARI MPYA

    Saturday, May 14, 2016

    KOCHA MPYA AZAM AMTABIRIA MEMA FARID HISPANIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya wa Azam FC, Jonas Garcia Luis amesema winga wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa Malik anaweza kuwa mchezaji mkubwa duniani baadaye.
    Akizungumza baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana jioni, Garcia alisema kwamba amemshuhudia Farid katika majaribio yake klabu ya Deportivo Tenerife nchini Hispania ni mchezaji mzuri.
    "Farid ni mchezaji mzuri sana, atasajiliwa Tenerife na atacheza Segunga (Daraja la Kwanza Hispania) na anaweza kuwa mchezaji mkubwa duniani,"alisema Garcia akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana JNIA.
    Makocha wawili kutoka klabu ya Deportivo Tenerife ya Hispania, Jonas Garcia Luis na Zebensul Hernandez Rodriguez  wamewasili jana jioni kwa ajili ya kuja kufanya mazungumzo ya kusaini Mkataba wa kufundisha Azam FC.
    Farid amefaulu majaribio katika klabu ya Deportivo Tenerife ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Hispania.
    Farid Mussa amefuzu majaribio klabu ya Deportivo Tenerife
    Mkurugenzi wa Azam FC, Yussuf Bakhresa aliyekuwa anafuatilia majaribio ya mchezaji huyo Hispania alisema Tenerife inatarajiwa kuingia katika mazungumzo na Azam FC juu ya kumnunua mchezaji huyo.
    “Tunatarajia kuanza mazungumzo nao juu ya suala la Farid, ingawa wazo lao la awali ni kumchukua kwa mkopo wa miaka miwili. Sasa tunasubiri ofa yao rasmi, kisha Bodi ya Ukurugenzi itajadili na kutoa maamuzi,”amesema Bakhresa.
    Kwa upande wake, Farid amefurahia matokeo hayo na kusema haikuwa kazi nyepesi kwake kuweza kuwaridhisha maofisa wa benchi la ufundi la Tenerife.
    “Kwa kweli nimefurahi sana na ninamshukuru Mungu kwa kufuzu majaribio, ila haikuwa kazi nyepesi, mpira wa Ulaya mgumu,”amesema.
    Jonas Garcia (kulia) akiwasili jana JNIA, katikati ni Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba na kushoto ni Rodriguez

    Awali, Farid ilikuwa apelekwe moja ya klabu za Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga, kati ya Las Palmas na Athletic ya Bilbao kwa majaribio, lakini wakala wake akashauri mchezaji huyo aanzie timu ya Daraja la Kwanza Hispania ili kupata nafasi ya kucheza na kuinuka haraka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MPYA AZAM AMTABIRIA MEMA FARID HISPANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top