• HABARI MPYA

    Friday, May 13, 2016

    KOCHA ARROWS AKUBALI MAVITU YA HAJIB, LAKINI ASEMA…

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini, Clinton Paul Larsen amevutiwa na uchezaji wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Hajib, lakini amesema anahitaji kumuona zaidi.
    Kocha huyo mzaliwa wa Durban, KwaZulu-Natal mwenye umri wa miaka 45, leo amekutana na Meneja wa mchezaji huyo wa Simba ya Tanzania na kumpa taarifa za awali.
    “Ameniambia anaonekana ni mchezaji mzuri, amevutiwa naye, ila anahitaji kuendelea kumuona zaidi kabla hajatoa majibu,”amesema Meneja wa Hajib, Juma Ndabila akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwa simu kutoka Durban.
    Kocha Clinton Paul Larsen (kushoto) akizungumza na Meneja wa Hajib, Juma Ndabila (kulia)

    Ndabila amesema Hajib alifanya vizuri katika mazoezi yake ya kwanza na timu hiyo jana na leo anaendelea tena.
    “Jana hadi wachezaji wa ile timu walimfuata na kuanza kumpa moyo, wanamuambia wewe mchezaji mzuri unaweza kusajiliwa hapa,”amesema Ndabile.
    Hajib yupo Afrika Kusini kwa ajili ya kusaka timu ya kuchezea, mipango inayosimamiwa na wakala maarufu nchini humo, Rodgers.
    Rodgers amewaalika Watanzania wawili kwa majaribio nchini humo, pamoja na Hajib mwingine ni kiungo chipukizi wa Azam FC, Omar Wayne ambaye tayari amefuzu majaribio katika klabu nyingine ya Ligi Kuu, AmaZulu.
    Hata hivyo, Wayne ameambiwa kutokana na umri wake mdogo inabidi asajiliwe kama mchezaji wa kikosi cha pili.
    Wayne mwenyewe amesema anaweza kukubali kusajiliwa AmaZulu B, lakini wasiwasi wake ni kama klabu yake, Azam FC itakubali kumtoa bure.  
    Mustakabali wa Wayne unatarajiwa kujulikana leo baada ya kikao cha viongozi wa AmaZulu.
    Hajib katika siku yake ya kwanza ya majaribio Green Arrows jana mjini Durban
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA ARROWS AKUBALI MAVITU YA HAJIB, LAKINI ASEMA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top