• HABARI MPYA

  Monday, May 02, 2016

  KAMUSOKO ‘AWAPIGIA SALUTI’ JUMA ABDUL NA NIYONZIMA, ASEMA VIJANA WANAJUA SOKA BALAA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa kimataifa wa Zimbabwe, Thabani Scara Kamusoko (pichani kushoto) amewasifu wachezaji wenzake wawili wa Yanga, beki Juma Abdul Mnyamani na kiungo Haruna Fadhil Niyonzima kwamba wana uwezo mkubwa kisoka.
  Kamusoko aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC baada ya kujiunga nayo kutoka Platinums FC ya kwao Julai mwaka jana, amesema Juma Abdul na Niyonzima, ambaye ni Nahodha wa Rwanda wana vipaji vikubwa.
  “Nimecheza mpira kwa muda mrefu, lakini hawa wachezaji wawili Juma Abdul na Haruna Niyonzima na miongoni mwa bora niliowahi kucheza nao,”amesema Kamusoko.
  Rasta huyo amesema wachezaji hao wana uwezo mkubwa kisoka na wanaweza kucheza popote duniani, zaidi ya Tanzania na Yanga.
  “Hawa wawili ni wachezaji wazuri miongoni mwa wazuri niliowahi kucheza nao, nawatakia heri Mungu awasaidie waweze kucheza kwa miaka mingi”amesema.
  Katika msimu wake wa kwanza tu Yanga, Kamusoko ametokea kuwa kipenzi cha wapenzi wa timu hiyo kutokana na msaada wake ndani ya kikosi cha wana Jangwani hao.
  Pamoja na kucheza nafasi ya kiungo akiwa mpishi wa mabao mengi yanayofungwa na washambuliaji wa timu hiyo, Mzimbabwe mwenzake Donald Ngoma na Mrundi, Amissi Tambwe, lakini naye Kamusoko  amefunga mabao nane katika mechi 46.
  Kesho, Kamusoko anatarajiwa kuichezea Yanga katika mechi ya 47 itakapomenyana na Stand United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Yanga SC inahitaji pointi saba katika mechi nne zilkizobaki ili kufikisha 72 na kutangaza ubingwa mapema, kwani haziwezi kufikiwa na timu nyingine.
  Mechi nne za Ligi Kuu za Yanga zilizobaki zote ni za ugenini tupu kuanzia dhidi ya Stand United kesho, Ndanda FC mjini Mtwara, Mbeya City mjini Mbeya na Majimaji mjini Songea baadaye. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMUSOKO ‘AWAPIGIA SALUTI’ JUMA ABDUL NA NIYONZIMA, ASEMA VIJANA WANAJUA SOKA BALAA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top