• HABARI MPYA

  Tuesday, May 17, 2016

  AVEVA: KESSY NA HAJIB WAMEISALITI SIMBA, AWALAUMU PIA NA TFF

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  RAIS wa Simba SC, Evans Aveva ametaja sababu kadhaa za timu hiyo kufanya vibaya msimu huu, mojawapo ni kuwa wachezaji wasio waaminifu baadhi yao beki Hassan Kessy na mshambuliaji Ibrahim Hajib.
  Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo hoteli ya Collessium, barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, Aveva amesema wachezaji hao walifanya vitendo ambavyo vimewaondolea uaminifu katika klabu.
  Aveva alisema Kessy alitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu na baada ya adhabu hiyo, klabu ikaamua kumuongezea adhabu, lakini kabla hajamaliza adhabu zake akaibuka anasaini kwa mahasimu Yanga.
  Ibrahim Hajib (kulia) akiwa na mchezaji wa Azam Fc, Omar Wayne waliyekutana kwenye majaribio Afrika Kusini

  Kuhusu Hajib, Aveva alisema mshambuliaji huyo alitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu pia na asubuhi yake akapanda ndege kwenda Afrika Kusini.
  Amesema mambo kama hayo pamoja na uendeshwaji mbovu wa Ligi Kuu unaofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) vimechangia Simba SC kufanya vibaya msimu huu. 
  Aveva amesema kutakuwa na Mkutano Mkuu wa klabu Julai 10, mwaka huu kujadili matatizo ya klabu na kutafuta suluhisho lake.
  Kauli ya Aveva inakuja Hajib amefuzu majaribio katika klabu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini.
  Hata hivyo, klabu hiyo haiko tayari kumnunua mchezaji huyo bali inataka kumchukua kama mchezaji huru na kumsainisha Mkataba.
  Kwa sababu hiyo, klabu hiyo imemuambia Hajib arejee Dar es Salaam kuangalia kama Mkataba wake umekwisha apeleke uthibitisho Afrika Kusini ili apewe Mkataba Arros.
  Wakala wa mchezaji huyo, Juma Ndabila ameiambia Lete Raha kwamba wanarejea leo Dar es Salaam pamoja na Hajib.
   “Amefuzu majaribio, lakini kuna suala la Mkataba hapa, yeye alisema kamaliza Mkataba, na Simba wanasema bado ana Mkataba, kwa hivyo anarudi kutatua hilo suala,”amesema Ndabila.
  Kwa upande wake, wakala aliyemuunganishia majaribio Hajib Afrika Kusini, Rodgers Mathaba amesema kwamba mchezaji huyo amepewa fursa ya kurudi Arrow wakati wowote akiwa mchezaji huru.
  “Amefuzu majaribio, sasa ni juu yake anatakiwa hapa kama mchezaji huru, anarudi Dar es Salaam kushughulikia Mkataba wake, nafasi yake ipo wazi hapa wakati wowote,”amesema Mathaba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AVEVA: KESSY NA HAJIB WAMEISALITI SIMBA, AWALAUMU PIA NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top