• HABARI MPYA

  Friday, April 15, 2016

  KAPOMBE AREJEA KUENDELEA NA MATIBABU NYUMBANI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amerejea nchini jana jioni baada ya wataalamu wa Hospitali ya Morningside Mediclinic ya jijini Johannesburg, Afrika Kusini kurishidhwa na maendeleo ya afya yake.
  Kapombe alikuwa jijini humo katika hospitali hiyo tokea Alhamisi iliyopita akipatiwa matibabu baada ya kugundulika anasumbuliwa na ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu) na sasa afya yake imezidi kuimarika hali iliyopelekea kuruhusiwa kutoka hospitali.
  Daktari Mkuu wa Azam FC, Juma Mwimbe amesema kwamba Kapombe amerejea nchini kwa sasa yupo kwenye mapumziko nyumbani kwake akiendelea na dozi ya dawa alizopewa na wataalamu hao wa Afrika Kusini.
  Shomary Kapombe (katikati) akikimbia baada ya kufunga katika moja ya mechi za Ligi Kuu msimu huu

  Mwimbe amesema Kapombe atakosekana uwanjani kwa kipindi chote kilichobakia cha msimu huu na huenda akarejea uwanjani wakati Azam FC itakapoanza kujiandaa na msimu ujao, lakini bado atakuwa akiendela na dozi aliyopewa kwani itamchukua si chini ya mwaka mmoja hadi miwili hadi kuweza kumaliza matibabu yote.
  “Hiyo haimaanishi atakuwa hachezi bali kutokana na madhara aliyopata na aina ya ugonjwa kitaalamu atahitaji kutumia dozi ya aina hiyo kwa muda usiopungua mwaka mmoja au  miwili ili mwili wake mzima urejee kwenye hali ya kawaida, lakini mara baada ya mapumziko ya miezi miwili hadi mitatu anayotakiwa kupumzika ataruhusiwa kucheza huku akiendelea na dozi,” alisema.
  Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, amekuwa na kiwango kizuri msimu huu kwani mpaka sasa ameshaifungia Azam FC mabao 11, nane kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), mawili Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na moja amepachika ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) wakati timu hiyo ikiilaza Bidvest Wits mabao 3-0. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAPOMBE AREJEA KUENDELEA NA MATIBABU NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top