• HABARI MPYA

  Monday, April 18, 2016

  BOSI WA BONDIA CHEKA ATAKA UONGOZI WA SOKA KINONDONI

  Na Majuto Omary, DAR ES SALAAM
  Meneja wa bondia Francis Cheka, Juma “Chief” Ndambile amesema kuwa ameamua kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa  Chama Cha Soka Cha Kinondoni (KIFA) kwa lengo la kuendeleza mchezo huu katika manispaa hiyo.
  Uchaguzi Mkuu wa Kifa umepangwa kufanyika Mei Mosi na utawashirikisha jumla ya wagombea 33 waliopitishwa na kamati ya Uchaguzi ya chama hicho.
  Ndambile ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni maarufu ya ulinzi yaAdvanced Security Co. Limited alisema kuwa kabla ya kuamua kuwania nafasi hiyo, alifanya uchunguzi wa kina na kugundua kuwa pamoja na Kinondoni kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji, tatizo kubwa ni uongozi.
  Ndambile alisema kuwa Kinondoni ina wadau wengi wa mpira wa miguu, lakini cha kushangaza mpaka sasa hakuna timu inayoshiriki LigiKuu ya Tanzania Bara na kubaki na timu za daraja la kwanza, pili na madaraja mengine ya chini.
  Alisema kuwa Kinondoni ina timu nyingi sana za mpira wa miguu ambazo zinaibua vipaji kutoka chini na wengine kuwa wachezaji wa kutegemewa wa timu za Ligi Kuu na timu ya Taifa, lakini kutokana na mfumo wa uongozi kuwa si mzuri, wachezaji hawa wanahamia timu nyingine na kuzipandisha daraja kucheza ligi kuu na Kinondoni kubakia nyuma.

  Mkurugenzi wa Kampuni ya Advanced Security  Limited, Juma Ndambile (wa kwanza kushoto) akiwa na bondia wake Francis Cheka  wakati wa kukabidhi mkanda wa ubingwa Super Middle kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Nape Nnauye (wa kwanza kulia).

   “Kungekuwa na uongozi bora ambao ungekuwa unafuatilia kikamilifu wachezaji na klabu, leo tusungekuwa na timu mbili tu daraja la kwanza, Friends Rangers na KMC zingekuwa ligi kuu na nyingi zingekuwa daraja la kwanza, sisi tumekuwa mishumaa wa kutoa mwanga huku tukiteketea,”
  “Siri kubwa ya kuondokana na hili ni kutafuta wadhamini kwa timu zetu na kuboresha hali ya wachezaji, Kinondoni ni Manispaa tajiri  Tanzania kwa kutumia wadhamini, waachezaji wangepata vipato vizuri na kupunguza kazi kwa viongozi kuhangaika huku na kule kusaka fedha za uendeshaji wa timu,” alisema Ndambile.
  Alifafanua kuwa mbali ya maslahi ya waamuzi, pia atahakikisha kunakuwa na uhusiano mzuri na vyama vishirikishi katika soka kama  madaktari wa michezo, makocha, soka la vijana, soka la wanawake, Suptanza na wadau wengine ili kujenga umoja wenye nguvu.
  Alisema kuwa yeye yupo tayari kufanya kazi wadau wote wa mpira wa miguu pamoja na kuhimarisha zaidi uhusiano wa serikali ya Manispaa ya Kinondoni na chama kwani ndiyo nyenzo pekee ya kufikia hatua kubwa kabisa ya maendeleo.
  “Sitakuwa kiongozi wa kukaa ofisini, kama mtendaji nitakuwa mfuatiliaji wa kila jambo kama ilivyo kwa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, tunahitaji kufanya kazi na si kutafuta sifa,” alisema.
  Mbali ya Ndambile, wagombea wengine katika nafasi hiyo ni Hashim Abdallah, Selemani Sufiani, Ramadhani Kampira, Funua Ally, Isack Mazwile na Raymond Solomon.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BOSI WA BONDIA CHEKA ATAKA UONGOZI WA SOKA KINONDONI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top