• HABARI MPYA

    Monday, April 18, 2016

    AYA 15 ZA SAID MDOE: TWANGA PEPETA MLIKUWA MNAFANYA MAKUSUDI?

    Onyesho la juzi usiku (Jumamosi) la The African Stars Band “Twanga Pepeta” pale Mango Garden, limenifanya niamini kuwa bendi hiyo ilikuwa inajipungizia yenyewe makali katika miaka ya hivi karibuni.
    Huko nyuma Twanga Pepeta iligeuka kero kwa watu wanaotaka burudani ya ukweli na badala yake ikabakia kuwa kivutio kwa wale tu wanazi wa bendi ambao hata ufanye madudu gani wao watasema hewala.
    Kwa miezi kadhaa iliyopita, Twanga Pepeta ilikuwa kama bendi yenye ukame wa nyimbo, asilimia 80 ya nyimbo utakazosikisikia kwenye maonyesho yao zilikuwa ni zile zile.
    Mbaya zaidi, nyimbo hizo zikawa zinarefushwa hadi zinachukiza, mwimbaji mmoja anarudia ‘pande’ lake mara nne – wimbo wa dakika 12 unageuka kuwa kuwa wa dakika 30 jukwaani!
    Kila baada ya nyimbo mbili lazima utasikia porojo kutoka kwa mmoja wa waimbaji, kuna wakati ulikuwa hata hujui ni nani anayepaswa kuwa msemaji kwenye maonyesho yao.
    Lakini onyesho la Jumamosi lilikuwa la aina yake, nidhamu ya jukwaani ilikuwa kubwa kiasi cha kushangaza, uchaguzi wa nyimbo (playlist) ukadhihirisha kuwa Twanga Pepeta ina utajiri wa nyimbo nyingi kali. Kwa upande wa masauti, kwangu mimi Chocky alikuwa nyota wa mchezo.
    Porojo za jukwaani zilipungua, mara chache sana alisikika Ally Chocky au Luizer Mbutu wakitangaza mambo muhimu juu ya onyesho lile au juu ya ratiba za show zijazo, lakini kinyume na hapo ilikuwa ni bandika bandua ya nyimbo kali tupu.
    Nyimbo hazikurefushwa ile ya kuchosha, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, nikawasikia mashabiki wa waliofika Mango Garden wakishangilia kila wimbo unapoanza kuashiria namna walivyokuwa wakikunwa na mpangilio wa nyimbo. 
    Haya ni baadhi ya mambo ambayo nimekuwa nikiyapigania sana, nimekuwa nikiandika sana juu ya mapungufu ya maonyesho ya bendi zetu kiasi hata cha baadhi ya wanamuziki kuanza kunichukia, lakini sasa naanza kupata imani kuwa kumbe licha ya kuchoma, lakini maoni yangu na ya wadau wengine yameanza kufanyiwa kazi (hata kama ni kwa mlango wa uani).
    Hivi Twanga Pepeta mlikuwa mnafanya makusudi? Raha kama za Jumamosi mlikuwa mnazibana kwa sababu gani? Sitegemei kama yaliyojiri Mango Garden juzi usiku yatakomea pale bali naamini ule ni mwanzo wa mabadiko ya kuishuhudia Twanga mpya.
    Kila bendi inahitaji kuwa kuwa na nyimbo mpya ili kuvuta wateja wapya, lakini pia inahitaji kulinda nyimbo zake kali za zamani zilizowapatia mafanikio, onyesho la Twanga Pepeta lilidhihirisha kuwa nyimbo za zamani si za kupuuzwa na zinapaswa kufanyiwa mazoezi ya kina. 
    Lakini pia mtu angewezaje kuondoka kwenye onyesho la Jumamosi bila kusifia ‘sound’ ya Twanga Pepeta!? Usikivu wa muziki uliotoka kwenye vyombo vyao ulikuwa ni mtamu, kitu ambacho kinanifanya pia nijiulize hizo siku nyingine Twanga mlikuwa mnafanya makusudi na vyombo vyenu?
    Waimbaji Luizer Mbutu, Haji BSS na Kalala Jr mara kadhaa walikwenda mbele kuungana na wacheza show na kwenda nao step kwa step, hapo pia najiuliza mlikuwa mnafanya makusudi kutofanya hivyo katika kila maonyesho yenu? Je waimbaji wengine wanafanya makusudi kutofanya yale yaliyofanywa na kina Haji BSS au wanaubeep uzee kwa nguvu?
    Tukiachana na mengi mazuri juu ya onyesho hilo, napata hamu kuuliza: Hivi Twanga Pepeta ule utaratibu wenu wa kuvaa pamba kali zinazofanana fanana rangi umeishia wapi? Onyesho maalum kama lile kwa kila msanii kutupiatupia pamba za kawaida kila mtu na rangi yake haikukaa poa, ila hongera kwa Kalala Jr alipendeza sana.
    Mwisho kabisa Twanga Pepeta inahitaji nyongeza ya mwimbaji kiraka (awe wa zamani au mpya), Twanga inahitaji kuboresha zaidi safu ya unenguaji ya wasichana, lakini pia kama katatokea kajinafasi kwa upande wa wanenguaji wa kiume, basi fumbeni macho mrejesheni Mandela, ana ladha yake jukwaani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: TWANGA PEPETA MLIKUWA MNAFANYA MAKUSUDI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top