• HABARI MPYA

  Friday, February 12, 2016

  YONDAN AFUNGIWA MECHI TATU NA KUPIGWA FAINI YA 'MALAKI' JUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Yanga SC, Kevin Yondan amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kumtupia usoni boksi la dawa, Daktari wa Coastal Union ya Tanga, Mganga Kitambi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu Januari 30, mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Hayo yamefrikiwa katika kikao cha Kamati ya Kusimamia na Kuendesha ligi (Kamati ya Masaa 72) kilichokutana Jumatano wiki hii kupitia taarifa mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza inayoendeea nchini.
  Na Yondan anayedaiwa kumtupia boksi Dk Kitambi wakati akimhudumia kipa wake katika, tayari amekosa mechi mbili hadi sasa dhidi ya Prisons na JKT Ruvu na atakosa pia mechi dhidi ya Simba SC, Februari 20, mwaka huu.

  Chanzi cha Yondan 'kumuadhibu' Dk Kitambi ni baada ya kumuomba maji daktari huyo, lakini akamnyima na adhabu huyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 na hata baada ya kumaliza adhabu ya kukosa mechi hizo, hataruhusiwa kucheza hadi atakapokuwa amelipa faini hiyo.
  Naye Dk. Kitambi anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kitendo chake cha kumrudishia Yondani kwa kumpiga ngumi. Kitendo cha Daktari huyo ni kinyume cha Kanuni ya 41(2), na pia Kanuni ya 36 kuhusu mchezo wa kiungwana.
  Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa Coastal Union walipokuwa wakishangilia bao la pili.
  Nayo klabu ya Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa washabiki wake kuvamia uwanja baada ya filimbi ya mwisho, kitendo ambacho ni kinyume cha Kanuni ya 14(11) inayohusu taratibu za mchezo.
  Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia chumba cha waandishi wa habari badala ya kile cha timu wakati wa mechi kati yao na Simba iliyochezwa Februari 3, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
  Kocha Ally Jangalu wa Coastal Union ameripotiwa kutoa matamashi ya kuidhalilisha TFF kwenye vyombo vya habari kuwa Refa wa mechi kati yao na Ndanda SC iliyochezwa mjini Tanga alikwenda na maelekezo ya kuhakikisha wapinzani wao wanashinda. Coastal Union ilifungwa bao 1-0 katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 4, 2016. Suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.
  Mchezaji Daud Jumanne amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumkanyaga vidole kwa makusudi mchezaji wa Simba aliyekuwa akisubiri kupatiwa matibabu kwenye mechi kati ya timu hizo iliyofanyika Februari 7, 2016 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
  Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015. Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 37(20), hauruhusiwi kucheza mechi inayofuata ya timu yake mpaka faini hiyo iwe imelipwa. Iwapo atacheza kabla ya kulipa faini hiyo, timu yake itapoteza mchezo husika.
  Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya African Sports iliyochezwa Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(13) kuhusu taratibu za mchezo.
  Kamishna wa mechi hiyo namba 140, Idelfonce Magali amepewa karipio kwa kutoripoti vizuri tukio hilo, wakati Refa Elly Sasii amepewa karipio kali kwa kutoripoti kabisa tukio hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YONDAN AFUNGIWA MECHI TATU NA KUPIGWA FAINI YA 'MALAKI' JUU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top