• HABARI MPYA

  Sunday, February 14, 2016

  ULIMWENGU: NATAKA KUWEKA REKODI MPYA KABISA AFRIKA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba kiu yake kwa sasa ni kuiwezesha klabu yake, Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutwaa taji la Super Cup la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  Baada ya kuipa Mazembe ubingwa wa Afrika, Novemba mwaka jana kwa kuifunga USM Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1, Ulimwengu sasa anatarajiwa kuiongoza timu hiyo mchezo wa kuunganisha mataji ya CAF, maarufu kama Super Cup dhidi ya mabingwa wa Kombe la Shirikisho, Etoile du Sahel ya Tunisia Februari 20, mwaka huu Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, DRC.
  Thomas Ulimwengu sasa anataka kuinua 'ndoo' ya Super Cup ya CAF

  Na akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana kutoka Lubumbashi, Ulimwengu alisema kwamba baada ya kuweka rekodi ya kuwa mmoja wa Watanzania wawili (pamoja na Mbwana Samatta) kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa anataka kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa taji la Super Cup la CAF.
  “Soka pamoja na yote, maslahi na kadhalika, lakini mwisho wa siku ni mchezo wa heshima na kumbukumbu. Ndiyo maana leo watu kama Pele, Maradona, Ronaldo (Lima) bado wanatajwa kutokana na rekodi walizoweka. Nami nitapenda pamoja na kuvuna fedha na heshima, lakini niweke kumbukumbu nzuri,”amesema.
  “Mimi na Samatta ni Watanzania pekee kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa na Afrika. Pia ni Watanzania pekee kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa. Pia ni Watanzania pekee kucheza Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA. Sasa wakati mwenzangu amenitangulia kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya, mimi nataka nimtumie picha nimebeba taji la Super Cup. Na nitakuwa Mtanzania wa kwanza kufanya hivyo,” amesema Ulimwengu.
  Ulimwengu na Samatta walicheza pamoja TP Mazembe kwa miaka minne, kabla ya mshambuliaji mwenzake huyo wa Tanzania kununuliwa na KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji Januari mwaka huu.
  Ulimwengu naye yuko mbioni kuhamia Ulaya mwishoni mwa msimu atakapomaliza Mkataba wake na kuna uwezekano akaenda kucheza Ligi Kuu ya Ufaransa au Ujerumani, ambako klabu kadhaa zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma zake.
  Lakini kabla ya kumenyana na Etoile Jumamosi ijayo, Ulimwengu anatarajiwa kuiongoza TP katika mchezo wa ugenini wa Ligi Kuu ya DRC Jumatano dhidi ya Saint Eloi Lupopo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU: NATAKA KUWEKA REKODI MPYA KABISA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top