• HABARI MPYA

    Friday, February 12, 2016

    SAFARI YA YANGA MAURITIUS YAANDAMWA NA MAJARIBU, TIMU HAIJAONDOKA, WACHEZAJI WAMEGANDA AIRPORT, KISA NDEGE MBOVU

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    SAFARI ya klabu ya Yanga SC kwenda Mauritius kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim imezidi kukumbwa na majaribu. 
    Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho Saa 9:30 Alasiri kwa saa za Mauritius Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam.
    Awali, Yanga SC ilipanga kuondoka Jumatano wiki hii, lakini ikaahirisha safari baada ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SA), kushindwa kuwapatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, kwenda mjini Curepipe.
    Kwa sababu hiyo, Yanga SC ikaachana na SA na kuamua kukodi ndege ya Shirika la Tanzania (ATC) ambayo walitarajiwa kusafiri nayo Alfajiri ya leo, lakini hadi sasa wachezaji wameganda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
    Sababu ni kwamba, ndege waliyotarajiwa kusafiri nayo imepata dosari kidogo – hivyo kwa sasa inafanyiwa marekebisho na matarajio ni timu hiyo kuondoka kuanzia jioni.
    “Tupo Uwanja wa ndege sasa, tunasubiri ndege yetu inafanyiwa marekebisho ndiyo tuondoke,”amesema Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro.
    Na alipoulizwa wanatarajiwa kuondoka saa ngapi, Mtangazaji huyo wa zamani wa ITV alisema; “Mchana hivi kwenye saa nane, au saa tisa (Alasiri),”. 
    Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ameamua kubeba kikosi chake chote kwa safari ya Mauritius, kwani baada ya mchezo huo Jumamosi, ndege hiyo ya ATC itaichukua timu hiyo kuipeleka Pemba, visiwani Zanzibar.
    Yanga SC itaweka kambi kisiwani Pemba, kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya mahasimu Simba SC, Februari 20, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga SC jana asubuhi ilifanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam kabla ya safari ambayo hadi sasa haina uhakika. 
    Mkuu wa Msafara anatarajiwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi, wakati upande wa viongozi wanakwenda Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu, Jerry Muro.
    KIKOSI KINACHOKWENDA MAURITUS;
    Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.
    Mabeki; Juma Abdul, Mbuyu Twite (DRC), Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Pato Ngonyani.
    Viungo ni; Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Issoufou Boubacar (Niger), Godfrey Mwashiuya na Deus Kaseke.
    Washambuliaji ni; Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).
    BENCHI LA UFUNDI; 
    Kocha Mkuu; Hans van der Pluijm (Uholanzi)
    Kocha Msaidizi; Juma Mwambusi
    Kocha wa Makipa; Juma Pondamali
    Daktari; Nassor Matuzya
    Meneja; Hafidh Saleh
    Mchua Misuli; Jacob Onyango
    Mtunza Vifaa; Mohammed Mpogolo
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAFARI YA YANGA MAURITIUS YAANDAMWA NA MAJARIBU, TIMU HAIJAONDOKA, WACHEZAJI WAMEGANDA AIRPORT, KISA NDEGE MBOVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top