• HABARI MPYA

  Friday, February 05, 2016

  PHIRI AWA KOCHA MPYA MBEYA CITY, MEJA MINGANGE 'ATUPIWA VIRAGO'

  KOCHA Mmalawi, Kinnah Phiri amesaini Mkataba wa miaka miwili kufundisha klabu ya Mbeya City ya Mbeya, ambayo imeamua kuachana na Meja Mstaafu, Abdul Mingange.
  Hatua hiyo inakuja baada ya kuona kikosi chake kinachoshiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara haina mwenendo mzuri tangu kuondoka kwa Juma Mwambusi aliyekwenda kuwa Msaidizi wa Mholanzi, Hans van der Pluijm Yanga SC.
  Meja Mingange aliyekuwa Msaidizi wa Mwambusi, amekuwa kaimu kocha Mkuu wa Mbeya City tangu Desemba, lakini sasa anaondoka moja kwa moja na Mohammed Kijuso ndiye atakuwa Kocha Msaidizi.
  Kinnah Phiri ndiye aliyefanikisha usajili wa Mrisho Ngassa klabu ya Free State ya Afrika Kusini 

  Mara ya mwisho Phiri ambaye ameiongoza timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) mara kadhaa alikuwa Afrika Kusini akiifundisha klabu ya Free State Stars inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo na ndiye aliyefanikisha usajili wa Mrisho Ngassa katika klabu hiyo ya Bethlehem.
  Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kwamba wana imani ujio wa kocha huyo mwenye uzoefu utasaidia kukijenga upya kikosi chao ambacho msimu huu kimekuwa na matokeo yasiyoridhisha.
  Kimbe alisema kwamba baada ya kukamilisha mazungumzo na kocha huyo mpya leo jioni anatarajiwa kuanza kazi yake ya kuanza maandalizi ya kukutana na mahasimu wao Tanzania Prisons hapo Jumapili.
  "Ni kweli tumepata kocha mpya, hatukuwa na amani pale timu ilipokuwa inafanya vibaya, tuliona tuna kila sababu ya kuboresha benchi la ufundi huku tukijipanga kuongeza wachezaji wengine mara baada ya msimu huu utakapomalizika," amesema Kimbe.
  Alitaja jukumu kubwa alilopewa Phiri ni kuhakikisha Mbeya City ambayo ina pointi 17 ikiwa katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi haishuki daraja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PHIRI AWA KOCHA MPYA MBEYA CITY, MEJA MINGANGE 'ATUPIWA VIRAGO' Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top