• HABARI MPYA

    Wednesday, February 03, 2016

    MSUVA AINUSURU YANGA SC KULALA KWA PRISONS, ASAWAZISHA KWA PENALTI, SARE 2-2


    Na Gwamaka Mwankota, MBEYA
    YANGA SC imezidi kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya 2-2 na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
    Matokeo hayo hayaiondoi kileleni Yanga SC ikifikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 17, mbele ya Azam FC na Simba SC wenye pointi 39 kila mmoja.
    Lakini Azam FC wana viporo wawili, wakati Simba SC ndiyo wamecheza mechi 17 kama Yanga. 
    Yanga SC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe aliyefunga kichwa akimalizia krosi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
    Kikosi cha Yanga SC kilichoanza leo Mbeya dhidi ya Prisons Uwanja wa Sokoine

    Prisons wakasawazisha bao hilo kupitia kwa Jeremiah Juma Mgunda aliyefunga kwa kichwa pia dakika ya 40 akimalizia krosi ya Mohammed Mkopi.
    Mkopi akaifungia Prisons bao la pili dakika ya 62 kwa kichwa pia akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo wa zamani wa Yanga SC, Juma Seif ‘Kijiko’.
    Mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Simon Msuva aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Deus Kaseke aliisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 84 baada ya beki Meshak Suleiman kuunawa mpira kwenye boksi.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Said Juma ‘Makapu’/Salum Telela dk59, Deus Kaseke/Simon Msuva dk54, Haruna Niyonzima na Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Issoufou Boubacar.
    Prisons; Benno Kakolanya, Benjami Asukile, Laurian Mpalile, James Mwasota, Nurdin Chona, Jumanne Fadhil, Lambert Sadianka, Freddy Chudu/Juma Seif dk48, Mohammed Mkopi, Jeremiah Juma na Leonce Mutalemwa/Meshack Suleiman dk51. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA AINUSURU YANGA SC KULALA KWA PRISONS, ASAWAZISHA KWA PENALTI, SARE 2-2 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top