• HABARI MPYA

  Wednesday, February 17, 2016

  MAYANJA: KWA MFUMO WAO, YANGA NITAWAPIGA HATA 3-0

  Na Princess Asia, MOROGORO
  KOCHA Mganda wa Simba SC, Jackson Mayanja amesema kwa mfumo wanaotumia Yanga SC anaweza kuwafunga hata mabao 3-0 Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.  
  Kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Uganda, aliyejiunga na Simba SC katikati ya Januari baada ya kuondolewa kwa Muingereza, Dylan Kerr amesema kwamba amekuwa akiifuatilia Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Hans van der Pluijm kwa muda mrefu, hususan kwenye michezo yao mitano iliyopita ya Ligi Kuu na haoni kwa nini asiwafunge Jumamosi.
  Mayanja aliyeiongoza Simba kushinda mechi zote sita za Ligi Kuu tangu atue Msimbazi akitokea Coastal Union ya Tanga, amesema kwamba anatambua umuhimu wa kushinda mchezo huo na anaamini itakuwa rahisi kwake kutimiza malengo hayo, iwapo wapinzani watacheza mfumo wao ule ule uliozoeleka wa 4-3-3.
  Kocha Jackson Mayanja wa Simba SC amesema anaweza kuwafunga Yanga SC hata 3-0

  “Sitaki kuonekana kwamba ninaleta maneno mengi, bali ninachokueleza ndiyo ukweli. Nimeisoma mifumo anayoitumia Pluijm Yanga na nimejaribu kutafuta mbinu za kutegua mbinu zake anazotumia. Pluijm kwenye michezo mingi amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3, ambao ni mfumo unaohitaji washambuliaji watatu wenye kuweza kucheza kitimu, lazima wawe na uwezo binafsi utakaowawezesha kuibeba timu inapozidiwa,”amesema kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar. 
  Mayanja ambaye enzi zake alichezea SC Villa na KCCA za kwao Uganda, amesema hana uhakika kama washambuliaji watatu wa Yanga SC, Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma, Amissi Joselyn Tambwe na Simon Happygod Msuva wanaweza kucheza mfumo huo ipasavayo. “Kama amekuwa akipata matokeo (mazuri) kwa mfumo huo, basi ni dhidi ya timu dhaifu na siyo Simba yangu,” amesema.
  “Bila kuwa na mfumo unaoendana na wachezaji wako ni kazi bure, kama Yanga wakiamua kutumia mifumo ambayo wamekuwa wakiitumia siku zote, basi kwangu nafakiri itakuwa sherehe. Ninaweza kutamba mapema nitawafunga hata mabao 3-0,” amesema. 
  Watani wa jadi, Simba SC na Yanga wanatarajiwa kukutana Jumamosi katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano.
  Mchezo wa kwanza Septemba 26, mwaka jana mabao ya Amissi Tambwe kipindi cha kwanza na Malimi Busungu kipindi cha pili yalitosha kuipa Yanga ushindi wa 2-0 dhdii ya watani wao hao wa jadi Uwanja wa Taifa.
  Simba SC imeweka kambi mjini Morogoro, wakati Yanga SC wapo kisiwani Pemba kwa maandalizi ya mchezo huo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAYANJA: KWA MFUMO WAO, YANGA NITAWAPIGA HATA 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top