• HABARI MPYA

  Thursday, February 18, 2016

  RIGOBERT SONG APEWA UKOCHA MKUU KIKOSI CHA CHAN CAMEROON

  NAHODHA wa zamani wa Cameroon, Rigobert Song amateuliwa kuwa kocha Mkuu wa kikosi cha wachezaji wa nyumbani wa Simba hao Wasiofungika, akichukua nafasi ya Martin Ndtoungou Mpile aliyeiongoza timu hiyo kwenye michuano ya CHAN mapema mwaka huu nchini Rwanda.
  Song, ambaye ametangazwa leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari ambao pia ulitumika kumtambulisha Hugo Broos kama kocha mpya wa kikosi kikubwa cha Cameroon, ataendelea pia kuwa katika benchi la Ufundi la timu ya kwanza ya Simba Wasiofungika.
  Ernest Agbor atakuwa Kocha Msaidizi wakati Simon Nlend atakuwa kocha wa makipa na Narcisse Tinkeu ataendelea kuwa kocha wa mazoezi ya viungo.
  Rigobert Song (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa Azam FC ya Tanzania, Yussuf Bakhresa (kulia) mjini Dar es Salaam mwaka 2012 alipokuja na kikosi cha Cameroon kama Meneja

  Cameroon ilitolewa kwenye Robo Fainali katika michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee baada ya kufungwa na Ivory Coast 3-0, mabao yote yakifungwa dakika za 30 za nyongeza baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 za kawaida.
  Na hiyo ilifuatia kuongoza Kundi B kwa kukusanya pointi saba baada ya kushinda mechi mbili 1-0 dhidi ya Angola 3-0 dhidi ya DRC na sare ya 0-0 na Ethiopia.
  Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 39, Song, anatarajiwa kuisaidia kwa uzoefu wake Cameroon kufuzu CHAN ijayo nchini Kenya mwaka 2018.
  Song ndiye mchezaji aliyeichezea mechi nyingi Cameroon, 137 na amecheza Fainali nne za Kombe la Dunia za miaka ya 1994, 1998, 2002 na 2010 pamoja na kuweka rekodi ya kucheza Fainali nyingi za Mataifa ya Afrika mara nane ambako amecheza jumla ya mechi 35.
  Ameshinda mataji mawili ya AFCON na Simba Wasiofungika mwaka 2000 wakiifunga Nigeria kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 2-2 na 2002 wakiifunga Senegal 3-2 kwa penalti pia baada ya sare ya bila kufungana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RIGOBERT SONG APEWA UKOCHA MKUU KIKOSI CHA CHAN CAMEROON Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top