• HABARI MPYA

    Monday, February 15, 2016

    HANS POPPE: HAKUNA RAHA KUBWA DUNIANI KAMA KUIFUNGA YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba; "Hakuna raha kubwa duniani kama kumfunga" Yanga SC.
    Hans Poppe amesema hayo jana akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kuelekea mpambano wa watani wa jadi, Simba na Yanga Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba Yanga lazima 'atafunwe' Jumamosi kwa sababu kubwa mbili, ambazo amezitaja ni kuwashikisha adabu watani na pia Simba kujiweka vizuri katika mawindo yake ya ubingwa.
    Zacharia Hans Poppe amesema kwamba hakuna 'raha kubwa duniani kama kuifunga Yanga"

    “Furaha ya kuwanyoa Yanga ni mara tatu ya furaha ya kawaida, kwani kipigo wanachopata watani wetu hao katika soka ni sherehe tosha kwa Simba, haswa kwa mbwembwe za mashabiki wetu,” amesema Hans Poppe.
    Simba SC imeweka kambini mjini Morogoro kujiandaa na mchezo huo, ikitoka kushinda mechi mbili mfululizo mjini Shinyanga 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na 2-1 dhidi ya Stand United.
    Mahasimu wao, Yanga SC wameweka kambi Pemba visiwani Zanzibar, wakitoka pia kushinda mechi mbili mfululizo, 4-0 dhidi ya JKT Ruvu katika Ligi Kuu na 1-0 ugenini dhidi ya Cercle de Joachim nchini Mauritius katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Ikumbukwe mchezo wa kwanza mwaka jana, Simba SC ilichapwa 2-0 mabao ya Malimi Busungu na Amissi Tambwe na Jumamosi ijayo watakuwa na deni la kulipa.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE: HAKUNA RAHA KUBWA DUNIANI KAMA KUIFUNGA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top