• HABARI MPYA

    Thursday, February 18, 2016

    HANS POPPE ATUA MAZEMBE KUCHUKUA MAMILIONI YA SAMATTA, ASEMA YANGA...

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe yupo Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) tangu jana kuchukua mgawo wao wa Euro 160,000 katika klabu ya TP Mazembe kutokana na mauzo ya mshambuliaji Mbwana Ally Samatta.
    Samatta alijiunga na Mazembe mwaka 2011 kwa dau la Sh. Milioni 100,000 akitokea Simba SC na Januari mwaka huu amejiunga na klabu ya Koninklijke Racing Club Genk ya Ubelgiji kwa Mkataba wa miaka minne na nusu.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kutoka Lubumbashi, Hans Poppe amesema kwamba ameteuliwa na klabu kwenda kuchukua fedha hizo, kufuatia wito wa Mazembe kuwataka Simba SC wakachukue haki yao.
    Hans Poppe (kushoto) akiwa na ofisini kwa Katibu wa TP Mazembe (kulia)
    Hans Poppe akiwa kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa TP Mazembe leo


    “Nipo hapa, mambo yanaenda vizuri, ninachukua mzigo fasta narudi Dar es Salaam kuimarisha nguvu ya maandalizi ya mchezo wetu na Yanga Jumamosi,”amesema Hans Poppe aliyefanikisha usajili wa Samatta mwaka 2010 kutoka African Lyon ya Dar es Salaam pia. 
    BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Samatta ameuzwa Genk kwa dau la Euro 800,000 Genk kutoka Mazembe ambayo inalazimika kuipa Simba SC asilimia 20 ya pato hilo kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Alipoulizwa kuhusu mchezo wao wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Yanga SC, Hans Poppe alisema; "Subiri kwanza nichukue huu mzigo hapa, nikirudi nitazungumza,". 
    Samatta aliyezaliwa Desemba 23, mwaka 1992, ameondoka Mazembe baada ya kushinda nayo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, ubingwa wa Ligi Kuu ya DRC mara nne na Super Cup ya DRC mara mbili.
    Ukiacha Euro 160,000, Simba SC pia inatarajia kulipwa pia dola za Kimarekani 300,000 za mauzo ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013.
    Samatta alitokea Simba SC kwenda TP Mazembe kabla ya kuuzwa KRC Genk
    Etoile wamekuwa wazito kulipa fedha hizo kwa sababu walidumu na Okwi kwa miezi sita kabla ya kushindwana na kushitakiana hadi FIFA.
    Etoile ilimtuhumu Okwi kuchelewa kurejea klabuni baada ya kuruhusiwa kwenda kuchezea timu yake ya taifa, wakati mchezaji akadai kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu. 
    Mwishowe Okwi aliruhusiwa na FIFA kutafuta klabu ya kuchezea wakati kesi yake na Etoile inaendelea – naye akarejea klabu yake ya zamani, SC Villa ya Uganda, ambayo baadaye ilimuuza Yanga SC mwaka 2014.
    Baada ya nusu msimu, Okwi akavurugana pia na Yanga hadi kufikishana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ambako aliruhusiwa kuondoka bure Jangwani, hivyo kujiunga tena na Simba SC kama mchezaji huru.
    Simba SC ikamuuza tena Okwi kwa dola za Kimarekani 100,000 klabu ya SonderjyskE ya Ligi Kuu ya Denmark, ambako anakoendelea na kazi hadi sasa. 
    Desemba mwaka jana, FIFA iliipa Etoile siku 60 kuwa imekwishalipa dola 300,000 za Simba SC, vinginevyo watachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa kucheza mashindano yoyote. 
    Na kuhusu fedha za Etoile, Hans Poppe amesema; "Watatulipa tu, hadi kufika Machi tutakuwa tumekwishapata fedha hizo,"amesema.
    Mbwana Samatta (kushoto) ndiye Nahodha wa Tanzania kwa sasa akiwa ana umri wa miaka 24 tu
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE ATUA MAZEMBE KUCHUKUA MAMILIONI YA SAMATTA, ASEMA YANGA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top