• HABARI MPYA

  Thursday, February 18, 2016

  CANNAVARO ASHINDWA KUENDELEA NA MAZOEZI PEMBA, YANGA YAREJEA KESHO DAR

  Na Suraiya Rahman, PEMBA
  NAHODHA wa Yanga SC, Nadir Haroub Ali 'Cannavaro' hayuko tayari kwa mchezo dhidi ya mahasimu, Simba SC Jumamosi, baada ya kushindwa kuendelea na mazoezi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
  Yanga SC, inatarajiwa kuondika mapema kesho kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao Simba SC, Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kambi ya wiki moja kisiwani Pemba.
  Jitihada za kocha Mholanzi, Hans Van Plujim kumshawishi Nahodha wake na beki tegemeo, Cannavaro kuendelea kufanya mazoezi ziligonga ukuta tangu jana, baada ya mchezaji huyo kutoka nje na kwenda kukaa katika benchi na kuwatazama wenzake wakiendelea na mazoezi.
  Hali hiyo imemuhuzunsha Pluijm ambaye Jumamosi atamkosa pia beki mwingine wa kati, Kevin Yondan anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu.
  Nadir Haroub 'Cannavaro' hayuko tayari kwa mchezo wa keshokutwa dhidi ya Simba SC

  Cannavaro amekuwa nje tangu Novemba mwaka jana, baada ya kuumia akiichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya wenyeji Algeria katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia.
  Na kulingana na maozezi ya jana na leo ya Yanga SC, kuna uwezekano nafasi za Yondan na Canvavaro zikazibwa na wageni, Mtogo Vincent Bossou na Mkongo, Mbuyu Twite. 
  Kikosi cha wachezaji 24 wa Yanga SC na viongozi sita kitaondoka kwa ndege maalumu ya kukodi katika Uwanja wa Pemba majira ya mchana kesho kurejea Dar es Salaam, ambako watafikia katika hoteli moja ya nyota tano katikati ya Jiji.
  Yanga ambayo imekuwa ikifanya mazoezi yake katika uwanja wa Gombani asubuhi na jioni kwa lengo la kuwaweka wachezaji wao vizuri, kabla ya mchezo huo wa marudiano wa Ligi Kuu, iliwasili hapa Jumapili ikitokea Mauritius ambako ilicheza mechi ya Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda 1-0 dhidi ya wenyeji, Vercle de Joachim.
  Yanga imeweza kubadilisha mazoezi yao ambayo walikuwa wakifanya jioni na sasa wanafanya asubuhi na jioni kwa muda wa siku mbili leo na kesho kabla ya kurudi Dar.
  Tangu timu hiyo iwasili kisiwani Pemba, imekuwa ikisumbuliwa na majeruhi mara kwa mara ya wachezaji wake, licha ya baadhi ya wachezaji Juma Abdul, Salim Telela na Simoni Msuva kupona majeraha yao na kuendelea na mazoezi.
  Yanga SC wakijifua Uwanja wa Gombani leo kabla ya kesho kurejea Dar es Salaam

  Katika mazoezi hayo kocha alionekana kuwaamini sana wachezaji wake kama vile Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Mwinyi Haji Mngwali, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke.
  Kocha mkuu wa timu hiyo amekuwa mkali sana kwa wachezaji hao wakati wanapokuwa katika mazoezi, huku akiwatumia kuwapa maelekezo sana wakati wanapokuwa mazoezini.
  Baadhi ya mashabiki kisiwani Pemba, wameridhishwa sana na mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea katika uwanja wa michezo gombani kisiwani Pemba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CANNAVARO ASHINDWA KUENDELEA NA MAZOEZI PEMBA, YANGA YAREJEA KESHO DAR Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top