• HABARI MPYA

  Saturday, January 02, 2016

  TFF: NIYONZIMA BADO MCHEZAJI HALALI WA YANGA SC, HATUTAMBUI KUVUNJIWA MKATABA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema halijapokea taarifa yoyote ya maandishi ya klabu ya Yanga SC kuvunja Mkataba na kiungo wake, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima (pichani kulia).
  Katika mahojiano na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Katibu wa TFF Mwesigwa Selestine amesema kwamba wao wamekuwa wakizisikia taarifa hizo kwenye vyombo vya habari tu.
  “Na kwa sababu hatujapata taarifa zozote rasmi, nasi hatuwezi kulizungumzia suala hilo, tunasubiri watakapotuletea taarifa, basi tutalifuatilia suala zima na kushauriana nao kwanza,”amesema.
  Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine (kulia) akiwa na Rais wa shirikisho, Jamal Malinzi

  Katibu huyo wa zamani wa Yanga SC, amesema kimsingi pande mbili zinapoingia Mkataba, linapofikia suala la kuuvunja upande mmoja hauwezi kuamua wenyewe, lazima upatikane upande wa tatu, ili kuonyesha juhudi za kulitatua suala zilifanyika,”.
  “Ngoja nikupe mfano wa ndoa, katika ndoa si mnaingia wawili, lakini wewe mmoja huwezi kusema basi imetosha. Lazima zifanyike juhudi, kwa hiyo mimi nadhani pande zote bado zina nafasi ya kufanya juhudi za kuokoa hii kitu,”amesema Mwesigwa.
  Katibu huyo wa TFF amesema hata suala hilo litakapofika kwao au likipelekwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kote huko lazima Yanga SC ikaonyeshe juhudi ilizofanya kutatua suala hilo kabla ya kufikia hatua hiyo.
  Mapema wiki hii, Yanga SC ilitangaza kuvunja Mkataba na kiungo wake, Haruna Niyonzima kwa madai kwamba kwa kipindi kirefu mchezaji huyo amekuwa akifanya mambo na kuonyesha tabia ambazo si za kianamichezo, gandamizi na ambazo zanaiathiri timu. 
  Ilidai Haruna amekuwa akirudia mambo hayo, licha ya klabu kumuonya mara kadhaa kwa barua na wakati mwingine kumkata mshahara na kwamba tabia zake zimekuwa zikiigharimu timu na klabu.
  Katika ufafanuzi wao, Yanga wamedai Haruna akichelewa na kukosekana mara kwa mara katika programu za timu, hususani anapokuwa amekwenda likizo au kutumikia timu yake ya Taifa ya Rwanda, ambako mara zote amekuwa akiondoka bila hata klabu kupata taarifa au kuombwa ruhusa. 
  Imemtuhumu pia kushiriki katika mashindano ambayo sio rasmi na bila kuruhusiwa na klabu, tu akiweka maslahi yake mbele na sio yale ya klabu.
  Kutokana na mambo haya manne, Yanga imedai Haruna ameshindwa kuishi kwa kufuata vipengele vya Mkataba wake kwa kushindwa kuthamini kazi yake na utovu wa nidhamu kwa programu za Yanga hususani mazoezi ya maandalizi.
  Aidha, Yanga SC imemtaka Haruna kulipa dola za Kimarekani 71,175 (Milioni 143)  kama gharama za kuvunja Mkataba na kwamba itapiga usajili wake popote bila kulipwa fedha hizo. 
  Wakati TFF ikisema haina taarifa rasmi, hata mchezo mwenyewe ameendelea kusema hajapewa barua rasmi ya kuvunjia Mkatana.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF: NIYONZIMA BADO MCHEZAJI HALALI WA YANGA SC, HATUTAMBUI KUVUNJIWA MKATABA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top