• HABARI MPYA

  Wednesday, January 06, 2016

  SIMBA WALIPASWA KUFIKIRIA MABADILIKO KABLA YA OFA YA DEWJI!

  MJADALA mkubwa unaoendelea kwenye vijiwe na matawi ya wana Simba ni ofa ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed ‘Mo’ Dewji kutaka kununua asilimia kubwa ya hisa za klabu.
  Mo Dewji ametoa pendekezo kwa uongozi wa Simba SC katika mazungumzo ambayo si rasmi baina yake na Rais wa klabu, Evans Elieza Aveva kununua hisa nyingi katika klabu ya Simba inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa lengo la kuwa mtu mwenye nguvu za umiliki.
  na Mo ambaye ni mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, amesema hataki kurudi Simba SC bila kupata manufaa, hivyo anashauri auziwe hisa.
  Kwa sasa Simba SC bado haijaingia katika mfumo wa kuuza hisa, inajiendesha kama klabu ya Ridhaa, inayomilikiwa na wanachama.

  Na ili kuingia katika mfumo wa kuuza hisa, lazima Mkutano Mkuu wa wanachama upitishe hilo na baada ya hapo mchakato uanze.
  Na hilo si jambo jepesi kama wengi wanavyofikiria, kutokana na uelewa mdogo wa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, hususan wale ambao wapo karibu na klabu.
  Kuna watu maisha yao ya kila siku yanakwenda kutokana na Simba SC na hao unapotaka kumpa mtu mmoja nguvu ya umiliki katika klabu watakuwa wapinzani wa awali wa mpango huo, kwa hofu ya kupoteza nafasi walizonazo chini ya mfumo wa sasa.
  Wazi, kama mtu mmoja atakuwa na nguvu za kimamlaka ndani ya klabu, ndiye atatengeneza mfumo mzima wa uendeshaji na utawala.
  Maana yake sasa kuna watu ambao kwa sasa maisha yanasababishwa na Simba SC watapoteza fursa hiyo na huo ni mtihani wa kwanza wa zoezi hilo.
  Mfano tu mahasimu wa jadi wa Simba SC – Yanga SC wao ndiyo walioanza vuguvugu la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu na mara nne zoezi hilo lilikwama.
  Kwanza, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga SC, George Mpondela ‘Castro’ alianzisha harakati hizo mwaka 1995, lakini hakufanikiwa na akageuka adui wa klabu.
  Mfanyabiahara Reginald Mengi alikuwa nyuma ya Mpondela katika wazo hilo naye kama Mo Dewji, alikuwa tayari kununua hisa nyingi. 
  Baadaye, Rais wa zamani wa klabu hiyo, Tarimba Abbas naye akajaribu, lakini ukatokea mgogoro mkubwa ndani ya klabu wa Yanga Kampuni na Yanga Asili ambao uliitafuna klabu kwa kipindi kirefu.
  Mengi alijaribu kuingia kusuluhisha mgogoro huo, lakini mwishowe akaambulia kudhalilishwa kwa maneno ya kashfa na wanachama mafedhuli.
  Rais mwingine wa zamani wa klabu hiyo, Francis kifukwe naye alijaribu bila mafanikio na hata Mwenyekiti wa sasa klabu hiyo, Yussuf Manji tangu bado mfadhili tu wa klabu, dhamira yake ni kutaka Yanga ijiendeshe kibiashara, lakini hadi leo hajafanikiwa.
  Unaweza kuona kwamba mpango huu ni mzuri, lakini una changamoto kubwa, ambayo ni kuwaelimisha wanachama ili wawe tayari kuukubali mfumo mpya.
  Haikuhitaji ofa ya Mo Dewji kwanza ndiyo Simba SC wafikirie mpango wa kujiendesha kibiashara, bali uongozi wowote wenye nia ya dhati ya kuifanya klabu siku moja iweze kuwa jeuri ya kujiendesha yenyewe ulipaswa kulifikiria hilo.
  Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeleta mageuzi makubwa katika mchezo kwa kutoa mwongozo wa sifa za viongozi na mfumo wa utawala, ikitaka wasomi ndiyo wapewe nafasi za kuongoza klabu na kuajiri sekretarieti za wataalamu.
  Sasa tumeondoka enzi za kuwa na Mweka Hazina, tuna Wakurugenzi wa Fedha, tumeondoka kwenye enzi za kuwa na Makatibu Mipango, tuna Watendaji Wakuu.
  Tumeondoka kwenye enzi za kuwa na Makatibu Wenezi, tuna Ofisa Habari na Mawasiliano – na pia tumeachana na desturi za kuchagua hata Wenyeviti wasiojua kusoma na kuandika, tuna wasomi wa viwango vya juu.
  Lakini pamoja na yote kuwa tayari yamekwishaingia nchini kwa zaidi ya miaka mitano sasa, lakini hatuoni matunda yake.
  Klabu bado zipo katika mfumo ule ule wa kizamani na hakuna jitihada za dhati za mabadiliko ya kimfumo.
  Simba na Yanga SC ni mihimili mikubwa sana katika soka ya nchi hii – lakini kwa kushindwa kwake kubadilika kuendana na wakati zimekuwa hazina faida.
  Tazama leo wana Simba SC wote wanashinda, wanakesha wanajadili ofa ya Mo Dewji kutaka kununua hisa nyingi za klabu, wakati bado wapo kwenye mfumo wa kizamani.
  Haikuhitaji ofa ya Mo Dewji kwanza ndiyo Simba SC waingie kwenye mchakato wa kutaka kujiendesha kibiashara.
  Weka kando ya ofa ya Mo Dewji, bali SImba SC sasa waamue wenyewe kwanza kubadilisha mfumo wa klabu na baadaye watangaze kuuza hisa. Watatokea akina Mo wengine wengi. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WALIPASWA KUFIKIRIA MABADILIKO KABLA YA OFA YA DEWJI! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top