• HABARI MPYA

  Thursday, January 14, 2016

  SIKU 10 ZILIZOONDOKA NA ‘ROHO’ YA MZUNGU WA SIMBA SC, WAGANDA WATAMBA TENA Z’BAR

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MICHUANO ya 10 ya Kombe la Mapinduzi, imefikia tamati kwa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) kutwaa ubingwa – huku kumbukumbu kubwa ikiwa ni kumponza kocha Muingereza, Dylan Kerr kupotea ajira yake Simba SC.
  URA yenye maskani yake Mji Mkuu wa Uganda, Kampala, imetwaa Kombe la Mapinduzi 2016 baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1 usiku wa jana Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Ushindi huo ambao unakwenda sambamba na kitita cha Sh. Milioni 10, unaifanya URA iwe timu ya pili ya Uganda kutwaa taji hilo, baada ya KCCA mwaka juzi.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mfaume Ali Nassor, hadi mapumziko, URA walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Wafalme; Wachezaji wa URA wakisherehekea na Kombe lao jana Uwanja wa Amaan 

  Bao hilo lilifungwa na Julius Ntambi kwa kichwa, akimalizia krosi ya Villa Oromchani kutoka upande wa kushoto.
  URA walikaribia kupata bao la pili dakika ya 37 baada ya Elkannah Nkugwa kupiga nje na kupoteza pasi ya Moor Semakula.
  Kwa ujumla, URA ilitawala mchezo na kuishika Mtibwa Sugar, ambayo safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Hussein Javu anayecheza kwa mkopo kutoka Yanga SC, iliishindwa kupasua ukuta wa wakusanya kodi wa Uganda.
  Kipindi cha pili, Mtibwa Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mecky Mexime ilijaribu kuongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la kusawazisha, lakini wakasahau kuongeza umakini wa kujilinda, hivyo kuwapa fursa URA kupata mabao mawili zaidi.
  Peter Lwasa aliyeingia dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Villa Oromchani, aliifungia URA mabao mawili ndani ya dakika tatu – kwanza dakika ya 85 baada ya kuunasa mpira uliopigwa fyongo na beki Dickson Daud na lingine dakika ya 88 akimalizia pasi ya Julius Ntambi.
  Jaffar Salum aliyeingia kuchukua nafasi ya Hussein Javu mwishoni mwa kipindi cha pili, aliifungia bao la kufutia machozi Mtibwa Sugar dakika ya 90, baada ya kuunasa mpira wakati kipa Brian Bwette anajaribu kumpiga chenga.
  Pamoja na kutwaa ubingwa, URA pia imetoa mfungaji bora, ambaye ni Peter Lwasa aliyemaliza na mabao matatu, akifuatiwa na Villa Oramchani wa URA pia, mabao mawili sawa na Awadh Juma wa Simba SC, Donald Ngoma wa Yanga SC, Mohammed Abdallah wa JKU na Kipre Tchetche wa Azam FC.
  Mtibwa Sugar wamepatiwa Sh. Milioni 5 kwa kushika nafasi ya pili. 
  Kiungo wa Simba SC, Justice Majabvi akipambana katikati ya wachezaji wa Mtibwa, Shaaban Nditi (kulia) na Salim Mbonde (kushoto)

  Vigogo, Simba na Yanga waliishia hatua ya Nusu Fainali, Yanga wakitolewa na URA kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, wakati Simba SC walitolewa na Mtibwa Sugar kwa kuchapwa bao 1-0.
  Wote, Simba na Yanga itabidi wajilaumu wenyewe kwa kutolewa kwao kabla ya mechi ya mwisho, kutokana na kuelekeza fikra zaidi kwenye fainali kabla ya kumaliza Nusu Fainali.
  Kwa ‘kuichukulia poa’ Mtibwa, Simba SC iliwaanzishia benchi wakali wake kadhaa wa kikosi cha kwanza wakiwemo, Hamisi Kizza, Ibrahim Hajib, Said Ndemla, Brian Majwega na Abdi Banda ili wasichoike kabla ya fainali, matokeo yake safari ikaishia hapo kwa bao la Ibrahim Rajab ‘Jeba’.
  Yanga SC kwa kuona ipo mbele kwa bao 1-0 hadi dakika ya 75, ikampumzisha mshambuliaji wake aliyekuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya URA, Donald Ngoma na dakika moja tu baadaye, Waganda wakachomoa kupitia kwa Peter Lwasa kabla ya kwenda kumaliza kazi kwenye matuta.
  Penalti za Yanga zilifungwa na Kevin Yondan, Deo Munishi ‘Dida’ na Simon Msuva huku Malimi Busungu na Geoffrey Mwashiuya wakikosa, wakati za URA zimefungwa na Deo Othieno, Said Kyeyune, Jimmy Kulaba na Brian Bwete, wakati Sam Sekito alikosa.
  Kipre Tchetche akiifungia Azam FC bao la kuongoza kabla ya Mafunzo kutoka nyuma na kushinda 2-1

  Timu nyingine iliyopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu, Azam FC nayo ilitolewa hatua ya makundi tu baada ya kufungwa mabao 2-1 na Mafunzo katika mchezo wa mwisho wa Kundi A.
  Azam FC nayo iliponzwa na kuwadharau wapinzani wao katika mchezo wa mwisho baada ya kupata bao la mapema la kuongoza, wakajikuta wanasawazishiwa na kufungwa la pili.
  Lakini pia, kitendo cha wachezaji wa Azam FC kuchagua mechi za kucheza kwa kujituma na nyingine kucheza kama wamelazimishwa kiliiponza pia timu kutolewa mapema.
  Wazi nguvu walizotumia wakati wanacheza na Yanga wakitoa sare ya 1-1 wangepata ushindi kama wangezitumia pia katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar wakitoa sare ya 1-1 na hiyo ya Mafunzo waliyofungwa.
  Michuano ya mwaka huu hajatokea mkali wa kutisha mabao, kwani mfungaji bora amemaliza na mabao matatu aliyofunga katika mechi mbili za mwisho, Nusu Fainali na Fainali.
  Peter Lwasa alimaliza mechi za makundi bila bao, akafunga bao lake la kwanza katika Nusu Fainali dhidi ya Yanga na akatokea benchi tena kuifungia mabao mawili URA katika fainali jana.
  Jumla ya mabao 33 tu yamefungwa katika mechi zote 15, huku kocha wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr na Msaidizi wake, Iddi Salim wakifukuzwa baada ya kutolewa katika Nusu Fainali.
  Wachezaji wa Yanga SC wakimpongeza Amissi Tambwe (kulia) baada ya kufunga bao la kuongoza dhidi ya URA

  Timu za Zanzibar zimeendelea kuwa wasindikizaji katika michuano hiyo ambayo wao ni wenyeji, safari hii zote zikitolewa hatua ya makundi tu. 
  Michuano ya mwaka ilikuwa ina msisimko zaidi tangu mwanzo, kutokana na timu za Simba na Yanga kuonyesha dhamira ya dhati ya kushiriki na kutumia vikosi vyao kamili.
  Hata hivyo, ladha ya mashindano ilikatika katika Nusu Fainali baada ya vigogo hao wote kutolewa na jana ikachezwa fainali iliyokosa msisimko. 

  WAFUNGAJI WA MABAO
  Mchezaji Timu Mabao
  Peter Lwassa URA               3
  Villa Oramchani URA               2
  Awadh Juma Simba SC 2
  Donald Ngoma Yanga SC 2
  Mohd Abdallah JKU 2
  Kipre Tchetche Azam FC         2

  Waliofunga bao moja kila mmoja; Ibrahim Hajib (Simba SC), Jonas Mkude (Simba SC), Vincent Bossou (Yanga SC), Paul Nonga (Yanga SC), Malimi Busungu (Yanga SC), Amissi Tambwe (Yanga SC), Oscar Agaba (URA), Emmanuel Martin (JKU), Said Kyeyune (URA), Nassor Juma (JKU), Mwalim Mohammed (Jamhuri) Ammy Mohammed (Jamhuri), Hussein Javu (Mtibwa), Shizza Kichuya (Mtibwa), Said Bahanuzi (Mtibwa), Ibrahim Jeba (Mtibwa), Jaffar Salum (Mtibwa) John Bocco (Azam FC), Habib Sadik (Mafunzo) Rashid Abdallah (Mafunzo).
  Kocha wa Simba SC, Dylan Kerr na kocha wa makipa Iddi Salim wamefukuzwa baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar katika Nusu Fainali

  MATOKEO NA RATIBA KOMBE LA MAPINDUZI 2016
  Jan 3, 2016
  Yanga SC 3-0 Mafunzo
  Mtibwa Sugar 1-1 Azam FC 
  Jan 4, 2016
  JKU 1-3 URA 
  Simba SC 2-2 Jamhuri 
  Jan 5, 2016
  Mafunzo 0-1 Mtibwa Sugar 
  Azam FC 1-1 Yanga SC 
  Jan 6, 2016
  Jamhuri 0-3 JKU 
  URA 0-1 Simba SC 
  Jan 7, 2016
  Azam 1-2 Mafunzo 
  Mtibwa Sugar 1-2 Yanga 
  Jan 8, 2016
  Jamhuri 0-1 URA
  Simba SC 1-0 JKU 
  Jan 10, 2016 - NUSU FAINALI 
  Simba SC 0-1 Mtibwa Sugar 
  Yanga SC 1-1 URA (URA imeshinda kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90)
  FAINALI; Jan 13, 2016
  Mtibwa Sugar 1-3 URA 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIKU 10 ZILIZOONDOKA NA ‘ROHO’ YA MZUNGU WA SIMBA SC, WAGANDA WATAMBA TENA Z’BAR Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top