• HABARI MPYA

  Sunday, January 10, 2016

  SAMATTA ALIONGOZANA NA WATU, AU ‘MIZIGO’ ABUJA!

  KAMA ilivyotarajiwa na wengi, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika katika sherehe zilizofanyika usiku wa Alhamisi ukumbi wa mikutano wa Kimataifa mjini Abuja.
  Samatta amepata pointi 127, mbele ya mchezaji mwenzake wa TP Mazembe, kipa Robert Muteba Kidiaba wa DRC, aliyepata pointi 88, wakati mshambuliaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia na timu ya taifa ya Algeria, Baghdad Bounedjah amepata pointi 63.
  Mafanikio ya Samatta anayeweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa ukanda w Afrika Mashariki na Kati kushinda tuzo kubwa ya Afrika, yanakuja baada ya kuiwezesha Mazembe kutwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake nane.

  Aidha, Samatta sasa ndiye anaweza kuitwa Mchezaji Bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania – bada ya miaka mingi ya kutokuwa na uhakika wa nani apewe sifa hiyo.
  Tunaweza kuwa na magwiji wengi, lakini wote sasa kimafanikio wanafunikwa na mtoto wa Ally Samatta, askari wa zamani wa jeshi la Polisi nchini.
  Lakini pamoja na ushindi huo wa Samatta, nchi imegubikwa na manung’uniko juu ya mapokezi ya shujaa huyo wa taifa.
  Wote walioingia fainali ya tuzo hizo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) walitumiwa tiketi na shirikisho hilo zenye muda wa kuondoka na kurudi.
  Na kwa kuwa katika watatu, yeyote angeweza kuibuka mshindi hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halikuwa na uhakika kama Samatta angeshinda.
  Kidiaba ni kipa namba moja wa DRC na TP Mazembe na Samatta ni mshambuliaji tegemeo wa klabu hiyo ya Lubumbashi na Tanzania.
  Hatuwezi kujilinganisha kimafanikio na DRC, lakini kwa mafanikio yoyote ya Mazembe, Samatta na Kidiaba wanahusika.
  Samatta alikuwa anafunga, Kidiaba anazuia Mazembe isifungwe na isingekuwa ajabu hata tuzo hiyo ingekwenda DRC.
  Mungu amesaidia, nyota imeangukia kwa kijana wetu. Tumshukuru Mungu kwa sababu pia kijana wetu alistahili ndiyo maana aliingia fainali.
  Ikumbukwe mshindi anapatikana kutokana na kura zinazopigwa na makocha au Wakurugenzi wa Ufundi wa Vyama au Mashirikisho ya soka ya nchi wanachama wa CAF.
  Nani angethubutu kusema tuandae sherehe na mapokenzi makubwa kabla ya Samatta kutangazwa mshindi – ungekuwa uchuro kama ule wa mwaka 1993 Simba SC walipotoa sare ya ugenini na Stella Abidjan ya Ivory Coast katika fainali ya kwanza ya Kombe la CAF na kuandaa tafrija ya kusherehekea Kombe, kabla ya kulitwaa.
  Zilitangazwa hadi barabara ambazo Kombe litapita kutoka Uwanja wa Taifa, matokeo yake Simba SC ikafungwa 2-0 nyumbani, mabao ya Boli Zozo na mwali akapaa Abidjan, siye tukibaki tumeduwaa na kushutumiana kuhujumiana.  
  Lakini TFF ilifanya jambo la maana kutoa mtu wa kuongozana na Samatta mjini Abuja na bahati nzuri baadhi ya Waandishi wa Habari wakasafiri pia.
  Kufika Abuja, msafara wa Samatta ukawa karibu na ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria na huko ndipo walipofanyiwa sherehe ya kwanza baada ya kushinda tuzo.
  Ajabu sasa, Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine aliyeongozana na Samatta, hao waandishi na hata Maofisa wa Ubalozi wote walikuwa kama mizigo, kwa sababu walishindwa kufikiria kwamba baada ya mchezaji huyo kushinda tuzo kuna haja ya kubadilisha muda wa kurejea kwake.
  Ni kweli, Samatta alipaswa kurejea mchana kweupe ili Watanzania wampokee kwa wingi, washerehekee naye na kumpongeza, lakini akarudi mida ile ile mibovu aliyopangiwa na CAF.
  Kumbe lilikuwa suala la watu waliokuwa naye Abuja kushauriana na Samatta, kisha wakawasiliana na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na hata Wizara ya Michezo juu ya kupanga muda mpya wa kurejea kwa mchezaji huyo apate mapokezi mazuri.
  Samatta kabla ya kuondoka alikutana na Waziri wa Michezo, Nape Nnauye na baada ya ushindi wake kila Mtanzania hata Rais, Dk John Pombe Joseph Magufuli alifurahia na kutoa pongezi.
  Ninaamini, kama watu waliokuwa na Samatta wangekuwa na vichwa vyepesi wangeweza kusaidia mchezaji huyo kubadilisha muda wa kurejea.
  Halikuwa suala la gharama tena za ziada labda za malazi, kula au tiketi za ndege za wote, Mwesigwa, waandishi na yeyote – lilikuwa suala la utaifa na ushirikishwaji wa Watanzania kwenye mapokezi ya shujaa wao.
  Basi kwa sababu walikuwa kule kama mizigo hawakuweza kufikiria lolote zaidi ya kupiga picha nyingi na Mbwana na kuposti kwenye Instagram na facebook.
  Yote kwa yote, wahenga wanasema maji yakishamwagika hayazoleki – tutaendelea kulaumiana, lakini hakuna kitakachobadilika.
  Niipongeze taasisi iliyojitolea kumtembeza Samatta jana mji wote wa Dar es Salaam kusherehekea na Watanzania tuzo yake, angalau ilikata kiu.
  Lakini pamoja na hayo, nataka niende mbali zaidi ya kufurahia tu tuzo ya Samatta.
  Mbwana Samatta ni mchezaji ambaye kama wachezaji wengi wa Tanzania aliibukia kwenye familia ya kawaida tu na alichezea timu za mtaani kabla ya kusajiliwa Mbagala Market, iliyobadilika na kuwa African Lyon na baadaye Simba SC.
  Akabahatika kusajiliwa na TP Mazembe mwaka 2011 na Mungu akamjaalia  nyota yake ikang’ara zaidi hatimaye sasa ni Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
  Sasa Samatta wakati wowote atatangazwa kujiunga na klabu moja ya Ulaya, kuanza harakati mpya za kusaka mafanikio zaidi. Mungu mkubwa, inawezekana siku moja akawa mchezaji mkubwa duniani.
  Ni wakati sasa wa wawekezaji na makampuni makubwa ya kibiashara nchini kujiuliza juu ya mchango wao kwenye michezo, kuliko tu kufurahia Samatta.
  Tunaweza tukabadilisha kabisa taswira ya soka yetu, iwapo tutawekeza na kusapoti miradi ya soka ya vijana kwa dhati ya nafsi zetu.
  Na itakuwa vyema sasa sisi wa vyombo vya Habari tukaanza kuhamasisha mabadiliko katika klabu kongwe nchini, Simba na Yanga ili ziwe katika mifumo ambayo itakuwa na tija kwa soka yetu kuliko ilivyo sasa.
  Lakini pia wakati umefika makampuni sasa yatumie wachezaji wa timu ya taifa katika matangazo yao ya kibiashara ili kuwainua kiuchumi.
  Samatta sasa ni bidhaa kubwa, ni faraja ya Watanzania – lakini tusiishie kwa Samatta tu, tuwafikirie na wengine ambao tunaamini wanaweza kufuata nyayo zake mfano Thomas Ulimwengu anayecheza naye Mazembe, Farid Mussa wa Azam na wengine.
  Zaidi ya yote, tuache kulaumiana kwa yaliyotokea – kila mmoja ameona kosa lake na tukubali kujifunza kutokana na makosa, tusonge mbele. Hongera Samatta. Hongera Sama Goal. Hongera Poppa! 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA ALIONGOZANA NA WATU, AU ‘MIZIGO’ ABUJA! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top