• HABARI MPYA

    Sunday, January 03, 2016

    NAMSHANGAA MO KUWABEMBELEZA SIMBA, AU KUPENDA NJIA ZA MKATO?

    MFANYABIASHARA Mohammed ‘Mo’ Dewji ameendelea kupambana na uongozi wa Simba SC katika mpango wake wa kutaka kuinunua klabu hiyo.
    Mara ya mwisho, Mo aliwapa Simba SC hadi Desemba 31 kuwa wamekwishatoa jibu la ndiyo hapana juu ya ombi lake la kutaka kuinunua klabu hiyo. 
    Tayari Mo ameweka wazi mpango wake wa kutaka kununua hisa nyingi katika klabu ya Simba inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa lengo la kuwa mtu mwenye nguvu za umiliki.

    Dewji alisema wazi yuko tayari kwenye mazungumzo na rais wa klabu hiyo, Evans Aveva ili kukamilisha mpango huo.
    “Unajua kila mtu ana interest, hakuna interest ya klabu, mimi nimeona sitaki nijihusishe na klabu ambayo haitafanikiwa, ndio maana mimi nilikuwa nasema Azam itakuja kufanya vizuri zaidi kuliko Simba na Yanga na wameanza,” alisema.
    “Nimeongea na rais wa Simba na ameniambia nimwandikie paper. Unajua mimi nimemwambia ‘wewe unafikiria mimi nikinunua hisa 51% ya Simba, maana yake nitaipeleka wapi? Mimi ni mtu wa hapa hapa na naipenda Simba. Leo mashabiki wa Manchester United, Arsenal they don’t care klabu ya nani, wanachohitaji ni mafanikio.
    Mimi nimewaambia nipo tayari niwekeze bilioni 20. Leo Katumbi wa TP Mazembe ni timu yake na inafanya vizuri. Mimi nimewaambia hata nikiwekeza bilioni 20 sitaona hela, mimi na biashara mia nyingine ninapata hela.
    Kwenye mpira ni mapenzi na timu basi. Tunataka kuendeleza mpira tuendeleze Simba yetu, tupate raha Simba ikishinda. Tayari nimeshamwandikia paper sasa tunakamilisha tutapeleka kama tutafanikiwa, kama ilishindika nitaanza na Mo Football Club,” aliongeza Mo.
    Aliongeza, “Tuliwafunga Zamalek, watu laki mbili walikuja kutupokea na bahati mbaya watu walikufa siku hiyo, sasa baada ya kushinda mimi niliitisha mkutano, nikasema jamani tumebahatika tumeshinda lakini hebu tujilinganishe na klabu ya Zamalek. Leo bajeti yetu ni shilingi ngapi na bajeti ya Zamalek ni shilingi ngapi? Leo Simba bajeti yake ni bilioni moja kwa mwaka it’s a joke!
    Mimi nimekuja na fikra nimesema kwamba jamani kwanini kuna watu wamesema wamejenga Simba? Tunawapa hisa bure za milioni 10 kila mmoja, tumefanya projection tunaweza kuraise zaidi ya bilioni 30 mpaka bilioni 40. Ukishapata bilioni 40 leo, ukienda kununua treasure bond unapata asilimia kumi tano.”
    “Sasa ukiwa na 40 bilioni , 10% ya 40 bilioni ni 4 na 5% ni 2 bilioni maana yake 6 bilioni. Unatoka kwenye 1 billion ya leo unaingia kwenye 6 bilioni, maana yake nini?
    Unaweza kumwajiri kocha mzuri, unaweza kuwa na gym pamoja na viwanja, unaweza kununua wachezaji ukashindana na Zamalek na hatimaye baada ya miaka mitano unaweza kushinda African Champions League,” alisisitiza.
    Hii si mara ya kwanza kwa Mo Dewji kuweka wazi mpango kama huu juu ya Simba, awali katika kipindi cha 1999 na 2005 wakati akiwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo, aliwahi kutoa wazo kama hilo.
    Alitaka Katiba ya Simba SC ibadilishwe na iwe kampuni ya kuuza hisa, ili anunie hisa nyingi za klabu hatimaye kuwa na nguvu za kimamlaka ndani ya klabu hiyo.
    Ukweli ni kwamba, siyo Simba tu – hata mahasimu wao, Yanga SC wapo katika mfumo wa kizamani mno ambao itachukua muda mno kufikia kwenye mabadiliko yatakayozalisha mafanikio.
    Wapenzi wa Simba na Yanga wanatamani sana kuona klabu zao zinapata mafanikio sawa na klabu nyingine maarufu barani Afrika kama TP Mazembe ya DRC, Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Esperance ua Tunisia, USMA Alger ya Algeria na nyingine nyingi.
    Lakini kwa mfumo wa uendeshwaji wa klabu zao ukweli kwamba ni vigumu mno kufikia ndoto hizo na – mabadiliko yanahitajika haraka.
    Wazo la Mo Dewji ndani ya Simba SC ndilo wazo ambalo mfanyabiashara mwingine, Reginald Abraham Mengi aliwahi kutoa kuhusu Yanga SC nyuma miaka ya 1990.
    Mengi naye alikuwa mfadhili wa Yanga SC miaka hiyo, akawasilisha wazo la klabu kuwa kampuni, ili iuze hisa kwa lengo la kujiendesha kibiashara.
    Na bila shaka kwa wakati huo, Mengi labda angekuwa mmiliki mkuu wa Yanga SC – kwani alionyesha dhamira ya kununua hisa nyingi.
    Lakini mwishowe alishindwa. Alishindwa kwa sababu ya uelewa mdogo wa wapenzi na wanachama wa Yanga wakati huo.
    Hicho ni kipindi ambacho hata klabu za England zilikuwa zinamilikiwa na Waingereza wenyewe – bado wawekezaji kutoka nchi mbalimbali hawajaingia, je watu wangemuelewaje Mengi?
    Na haikushangaza Mengi ambaye bila shaka ni mpenzi wa Yanga SC aliondoka vibaya katika klabu hiyo. Alifanyiwa fujo na wanachama katika Mkutano uliofanyika ukumbi wa Star Light Cinema mwaka 1999.
    Nasikitika, hadi leo Yanga SC hawajafikiria kwenda kumuomba radhi Mengi – lakini ukweli ni kwamba huyo ndiye aliyekuwa mkombozi wa kwanza wa kweli wa klabu yao.   
    Watazame Yanga SC, kwa sasa jeuri yao inatokana na Mwenyekiti na mfadhili wao, Yussuf Manji – huyo akiondoka tu maisha yao yatakuwa ya tabu sana hadi atokee mkombozi mwingine sijui lini!
    Watu wepesi tu wa kusahau tu, lakini Manji aliikuta Yanga katika hali mbaya mno chini ya Rais Francis Kifukwe.
    Yanga ilifikia kuwa timu ya kuweka kambi katika nyumba za kulala wageni huko Boko na kuchangiwa fedha na mashabiki jukwaani. Watu wamesahau.
    Yote kwa yote, niseme namshangaa Mo Dewji kuwabembeleza Simba SC, wakati akiamua ndani ya miaka mitano anaweza akawa na klabu yake imara kuliko Simba na Yanga.
    Naona kama Mo anapenda njia za mkato, lakini kama anaamua kuwekeza na kuwa mwenye subira – miaka mitano mingi anakuwa mshindani wa Azam FC.
    Na hiyo maana yake nini sasa? Simba SC itazidi kupotea kwenye ramani na Yanga SC kwa jeuri ya Manji watakuwa wamepata mshindani mwingine, baada ya Azam.
    Ikitokea tu Manji akawaachia Yanga yao na upande wa pili Mo akasimamisha klabu yake madhubuti – basi tutaanza kuhesabu siku kuelekea mwisho wa utawala wa vigogo hao katika soka ya Tanzania. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NAMSHANGAA MO KUWABEMBELEZA SIMBA, AU KUPENDA NJIA ZA MKATO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top