• HABARI MPYA

  Thursday, January 07, 2016

  MAFUNZO YAIFUNGISHA VIRAGO AZAM FC, YANGA NA MTIBWA ZATINGA NUSU FAINALI

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  KWA mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Mapinduzi, Azam FC imetolewa katika hatua ya makundi, baada ya kufungwa mabao 2-1 jioni ya leo na Mafunzo FC Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Azam FC pia inaondoka bila ya ushindi katika mashindano hayo, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia yake ya ushiriki wa michuano hiyo ikimaliza na pointi mbili, za sare dhidi ya Yanga na Mtibwa Sugar, zote 1-1 pamoja na kipigo cha leo. 
  Aliyewarudisha mapema Azam FC Dar es Salaam leo ni Habib Sadik aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Haji Abdi dakika ya 90 na ushei kuipatia Mafunzo bao la pili.
  Azam FC walitangulia kupata bao kupitia kwa mshambuliaji Kipre Herman Tchetche dakika ya 20 akimalizia kona iliyochongwa na beki wa kulia, Shomary Kapombe.
  Sadik Habib (kulia) akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la pili dakika za lala salama

  Mafunzo ambao leo walicheza bila kocha wao Mkuu, Hemed Morocco, aliyefiwa na mama yake mzazi, ilipata bao la kusawazisha dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake, Rashid Abdallah  aliyemalizia pasi ya Ali Hassan.
  Matokeo haya yanazifanya Yanga SC na Mtibwa Sugar zenye pointi nne kila moja zifuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali na zitamenyana katika mechi ya mwisho ya kundi A usiku wa leo kusaka mshindi wa kwanza na wa pili.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Ivo Mapunda, Shomary Kapombe/Khamis Mcha dk 79, Erasto Nyoni, Serge Wawa, Abdallah Kheri, Farid Mussa/Ramadhani Singano dk65, Abubakar Salum, Mudathir Yahaya/Frank Domayo dk65, Allan Wanga, Kipre Bolou/Ame Ali dk69 na Kipre Tchetche.
  Mafunzo; Khalid Haji, Juma Mmanga/Kheri Salum dk 10, Haji Mwambe, Haji Hassan, Said Shaaban, Ali Hassan/Jermaine Seif dk58, Samih Nuhu/Ahmed Maulid dk84, Hassan Juma, Abdulaziz Makame, Rashid Abdallah na Shaaban Ali/Sadick Habib dk72.
  Mshambuliaji wa Azam FC akimtoka beki wa Mafunzo, Abdulaziz Makame wa Mafunzo

  Kipre Tchetche akienda hewani kuifungia Azam FC bao kuongoza 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAFUNZO YAIFUNGISHA VIRAGO AZAM FC, YANGA NA MTIBWA ZATINGA NUSU FAINALI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top