• HABARI MPYA

  Tuesday, January 05, 2016

  HANS POPPE ATOA MSIMAMO WAKE MPANGO WA MO DEWJI KUINUNUA SIMBA SC, ASEMA…

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba anaunga mkono klabu kuingia katika mfumo wa kuuza hisa.
  Katika mahojiano na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo mchana ofisini kwake, Mbezi Beach, Dar es Salaam, Poppe amesema pia anaafiki Mohammed ‘Mo’ Dewji kununua asilimia kubwa ya hisa za klabu.
  Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba naye atanunua hisa iwapo klabu itafanikiwa kuingia katika mfumo huo wa kisasa.
  “Nimelazimika kuelezea msimamo wangu huu baada ya kuibuka kwa vikundi vya watu vikisambaza habari za upotoshaji kwamba mimi napinga Mo kununua hisa nyingi za klabu,”amesema.
  Zacharia Hans Poppe amesema anaunga mkono mabadiliko ya mfumo Simba SC

  Aidha, Poppe aliyekuwamo kwenye vikosi vya askari wa JWTZ walioyapiga majeshi ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Iddi Amin ‘Dada’ (sasa marehemu) yaliyovamia sehemu ya Tanzania mkoa wa Kagera amewaonya wanaosambaza habari za uongo dhidi yake, wakiendelea atawachukulia hatua za kisheria.
  “Kusema eti mimi nilikaa kikao na Wazee (wa Simba) kupinga Mo kununua hisa nyingi za klabu ni uongo, kwa sababu mimi nilikuwa Iringa tangu Desemba 24 hadi Januari 4 ndiyo nimerudi Dar es Salaam. Sasa nilikutana lini na hao wazee?”amehoji.
  Pamoja na hayo, Poppe amesema madai kwamba hataki Mo anunue hisa nyingi Simba SC kwa sababu itashindikana kulipwa fedha zake alizotumia kusajili nayo ni uzandiki mtupu.
  “Mimi siudai hata senti uongozi huu wa Simba SC uliopo madarakani. Fedha ambazo bado ninadai ni wakati wa uongozi wa Rage (Alhaj Ismail Aden) nilitoa fedha za kusajiliwa Emmanuel Okwi (dola za Kimareani 40,000, zaidi ya Sh. Milioni 80) ambazo tulikubaliana nitalipwa akiuzwa Etoile du Sahel,”.
  “Nasi sote tunajua kwamba zile fedha hadi leo hazijalipwa. Sina wasiwasi, najua Etoile wakilipa, nami nitapewa haki yangu. Sasa nawatahadharisha watu wanaosema maneno ya uongo, waache, vinginevyo nitawachukulia hatua na wasije kunilaumu,”amesema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE ATOA MSIMAMO WAKE MPANGO WA MO DEWJI KUINUNUA SIMBA SC, ASEMA… Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top