• HABARI MPYA

    Thursday, January 14, 2016

    HANS POPPE ATAJA SABABU ZA KUIJENGEA SIMBA UWANJA, AIPONGEZA SERIKALI KUMPA SAMATTA KIWANJA KIGAMBONI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba anajitolea kuijenga Uwanja wa mazoezi klabu hiyo kwa mapenzi yake.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE, Hans Poppe amesema kwamba amekuwa akiumia sana kuona Simba SC inahangaikia Uwanja wa kufanyia mazoezi wakati tayari ina eneo lake Bunju.
    “Nilikaa nikatafakari gharama za ujezi wa Uwanja mzuri wa mazoezi, nikaona ninaweza kuifanyia kitu hiki klabu yangu. Na sasa nipo katika mchakato wa kuanza ujenzi muda si mrefu,”amesema Poppe.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba anataka Simba SC iondokane kabisa na tatizo la Uwanja wa mazoezi.
    Zacharia Hans Poppe amejitolea kwa mapenzi yake kuijengea Simba Uwanja wa mazoezi 

    “Sitapenda kuendelea kuona tunahangaikia Uwanja wa mazoezi, ndiyo maana nimeamua kujitolea kwa mapenzi yangu kuwajengea Uwanja wa mazoezi,”amesema.    
    Pamoja na hayo, Poppe ameipongeza Serikali kwa kumpa zawadi ya kiwanja, mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Mbwana Samatta baada ya kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
    “Nichukue fursa hii pia kuipongeza Serikali kwa kumpa Samatta kiwanja baada ya heshima kubwa aliyoiletea Tanzania, nasikia wamempa na fedha pia. Ni vizuri sana. Na ninadhani hii itawaamsha na wachezaji wengine waongeze bidii,”amesema.
    Juzi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alimkabidhi Samatta anayechezea TP Mazembe ya DRC hati ya kiwanja kilichopo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam pamoja na bahasha ya fedha, ambazo hata hivyo kiwango chake hakikutajwa.
    Kwa sasa Samatta yuko mbioni kujiunga na klabu ya KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji na tayati Ubalozi wa nchi hiyo hapa Tanzania umempatia viza ya kwenda huko kukamilisha usajili wake.

    Samatta akiwa na bahasha ya burungutu la fedha alilokabidhiwa na Waziri wa Nyumba Ardhi na Maendelea Wiliam Lukuvi (kushoto) pamoja na hati ya kiwanja (katikati) ni Waziri wa Habari na Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye

    Ingawa bado klabu yake, TP Mazembe haijatangaza rasmi, lakini taarifa zinasema mwishoni mwa mwaka jana, Rais wa klabu hiyo ya Lubumbashi, Moise Katumbi alifikia makubaliano na klabu hiyo ya Ubelgiji juu ya biashara ya mchezaji huyo.
    Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, anaondoka Mazembe baada ya kuichezea mechi 103 na kuifungia mabao 60.
    Kijana huyo wa umri wa miaka 24, anaondoka Mazembe akiiachia taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE ATAJA SABABU ZA KUIJENGEA SIMBA UWANJA, AIPONGEZA SERIKALI KUMPA SAMATTA KIWANJA KIGAMBONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top