• HABARI MPYA

    Wednesday, January 01, 2014

    SIMBA SC YAUANZA VYEMA 2014, YAICHAPA LEOPARD 1-0 KOMBE LA MAPINDUZI

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    BAO pekee la kiungo Amri Ramadhani Kiemba, usiku huu limeifanya klabu ya Simba SC iuanze vyema mwaka 2014 baada ya kuifunga AFC Leopard ya Kenya 1-0 katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Mapinduzi, Kundi B, Uwanja wa Amaan, Zanzibar. 
    Simba wakishangilia bao lao pekee leo Uwanja wa Amaan
    Kiemba aliyetokea benchi dakika ya 47 kwenda kuchukua nafasi ya Awadh Juma Issa, alifunga bao hilo baada ya kuunasa mpira uliookolewa na beki wa Leopard, kufuatia Amisi Tambwe kujaribu kuunganisha krosi ya Ramdhani Yahya Singano ‘Messi’ dakika ya 77.  

    Sifa zimuendee Messi, ambaye alimlamba chenga ya maudhi beki ngongoti, Joseph Shikokoti kabla ya kutia krosi iliyozaa bao hilo.  
    Kwa ujumla Simba SC, ambayo leo ilioongozwa na kocha Msaidizi, Suleiman Abdallah Matola ilicheza vizuri zaidi kipindi cha pili na ingeweza kuondoka na ushindi mnene kidogo, kama washambuliaji wangekuwa makini zaidi. 
    Leopard nayo ilicheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza, safu yake ya kiungo ikiongozwa na mkongwe Oscar Kadenge.
    Kwa ushindi huo, Simba SC inashika nafasi ya pili katika Kundi B kwa pointi zake tatu, nyuma ya KCC ya Uganda yenye pointi tatu pia, ambayo iliilaza KMKM 3-2 katika mechi ya kwanza jioni ya leo.
    Kocha wa timu ya taifa ya Italia, Cesare Prandile aliyekuwa mgeni rasmi, alikagua timu zote mbili kabla ya mechi hiyo na kwenda kuudunda mpira katikati ya Uwanja kuashiria ufunguzi wa michuano hiyo ya nane ya Kombe la Mapinduzi. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rid, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Ramadhani Chombo/Uhuru Suleiman dk89, Amisi Tambwe/Betram Mombeki dk81, Ramadhan Singano, Awadhi Juma/Amri Kiemba dk47.
    AFC Leopard; Martin Masalia, Etenesy Augustin, Abdallah Juma, Saleh Jackson, Joseph Shikokoti, Imbalebala Martin, Okwemba Charles, Mussa Mude, Kelly Jacb, Mang’ole Benard/Seda Edwin dk86 na Oscar Kadenge/Hassan Mohamed dk86.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAUANZA VYEMA 2014, YAICHAPA LEOPARD 1-0 KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top