• HABARI MPYA

    Sunday, July 07, 2013

    STEWART 'AMCHINJIA BAHARINI' KASEJA AZAM, ASEMA MWADINI NA AISHI WATOSHA SANA

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 7, 2013 SAA 3:39 ASUBUHI
    KOCHA Mkuu wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amekiri Juma Kaseja ni bonge la kipa, lakini amesema kwamba sasa anataka Aishi Manula na Mwadini Ally wapambane kuwania nafasi ya kipa wa kwanza wa timu na hana mpango wa kusajili kipa mwingine.
    Muingereza huyo amesema kipa wake mwingine, Jackson Wandwi anampeleka kucheza kwa mkopo Ashanti United ya Ilala iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, ili kukusanya uzoefu baadaye arejee kushindana na Mwadini na Aishi.
    Hatumuhitaji Kaseja; Stewart Hall kulia akiwa na Msaidizi wake, Kali Ongala

    “Najua Kaseja ameachwa Simba SC, na nasikia watu wanamzungumzia sana wakimhusisha na Azam. Mimi nakubali yule ni kipa mzuri na ana uzoefu. Ila mimi nina makipa wazuri wawili, Aishi na Mwadini. Nataka hawa wagombee kuwa kipa wa kwanza wa timu,”alisema.
    Hall amesema kwamba bado Azam ina makipa wengine wazuri wa timu za vijana, ambao watakuwa wakipewa nafasi ya kujifua na kikosi cha kwanza msimu ujao.
    “Kama nitakuwa na Aishi na Mwadini kama makipa wawili imara wa timu ya kwanza, maana yake Wandwi ataendelea kuua kiwango chake. Nimeona bora nimpeleke Ashanti ili akakusanye uzoefu, baadaye arejee kwenye timu akiwa imara,”alisema.
    Azam wakiwa mazoezini ufukwe wa Coco Dar es Salaam jana. Wandwi (katikati) anapelekwa kwa mkopo Ashanti United.

    Aidha, kuhusu maandalizi ya msimu mpya, Hall amesema kwamba kwa sasa Azam ambayo itaiwakilisha Tanzania kwa mara ya pili mfululizo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, iko katika mazoezi.
    “Tunaendelea na mazoezi ya msimu mpya. Kwa sasa tupo katika programu ya ufukweni na gym. Baada ya hapo tutaanza programu rasmi ya uwanjani. Lakini wiki mbili za mwanzo za Agosti tutakwenda Afrika Kusini kuweka kambi,”.
    “Tukiwa huko tutafanya mazoezi katika Uwanja mzuri na kupata mechi nne za kujipima nguvu dhidi ya timu kama Orlando Pirates, Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundwons na nyingine,”alisema.
    Aishi Manula atagombea namba na Mwadini Ally

    Hall amesema kwamba baada ya hapo watarejea Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu, Yanga SC.     
    “Lengo letu ni kutwaa mataji yote msimu ujao. Tumekuwa washindi wa pili mara mbili mfululizo katika Ligi Kuu, sasa huu ni wakati wa kutwaa taji. Mwaka jana tumeikosa Ngao, lakini mwaka huu tunataka kuchukua. Katika michuano ya Afrika tunataka kuvuka hatua tuliyofika mwaka huu (16 Bora) na tucheze Nane Bora, hiyo ndiyo mikakati,”alisema.
    Mwadini Ally atatakiwa kudhihirisha uwezo wake aendelee kuwa kipa namba moja Azam, vinginevyo atapokonywa namba na Aishi
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: STEWART 'AMCHINJIA BAHARINI' KASEJA AZAM, ASEMA MWADINI NA AISHI WATOSHA SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top