• HABARI MPYA

  Sunday, July 07, 2013

  GARI LAKWAMISHA USAJILI WA KIIZA YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 7, 2013 SAA 12:04 ASUBUHI
  HAMISI Friday Kiiza, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda yu tayari kusaini Yanga SC kwa dau la dola za Kimarekani 40,000 na mshahara wa dola 1,500 kwa mwezi na klabu ipo tayari kumtekelezea hayo, lakini kuna kitu kinakwamisha mpango huo.
  Kiiza anataka apewe fedha taslimu dola 40,000 wakati Yanga inamlazimisha achukue dola 35,000 na dola 5,000 nyingine apewe gari, kitu ambacho Diego hataki, anataka fedha.
  Sitaki gari, nataka dola 40,000; Hamisi Kiiza kushoto akizungumza na Bin Kleb kulia baada ya kuwapa raha wana Yanga katika mechi ya kufunga msimu uliopita kwa kufunga bao zuri dhidi ya watani, Simba SC. 

  Mchezaji huyo wa Uganda anaweza kuondoka kwa sababu ya kulazimishwa kuchukua gari katika sehemu ya dola 40,000 za kusaini Mkataba mpya, wakati yeye anataka fedha tupu. 
  Kiiza anaishi Uganda na Tanzania yupo kwa ajili ya kazi na haoni umuhimu wa kumiliki gari Dar es Salaam, hivyo anataka fedha, lakini watu wanaohusika na usajili Yanga inadaiwa wanamlazimisha achukue na gari. 
  Mashabiki wa Yanga wana hamu ya kuendelea kumuona Kiiza anaitumikia timu hiyo, lakini kuna uwezekano asirejee msimu ujao baada ya kumaliza Mkataba wake wa miaka miwili.

  Kifaa kinaondoka; Hamisi Kiiza kulia akiichezea Yanga msimu uliopita.

  Hiyo inatokana na mvutano wa mahitaji katika Mkataba wake mpya, yeye akitaka fedha tupu, lakini wanaohusika na usajili wanataka achukue na gari.
  Tayari Yanga SC inaonekana kuwa katika harakati za kutaka kusajili mshambuliaji mwingine kuziba pengo la Kiiza na baada ya kumkosa Mganda Moses Oloya anayecheza Vietnam inaonekana kupigania saini ya mshambuliaji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Javu.
  Dau la jumla la kumsajili Javu linaweza kufika dola 50,000 kwa maana ya fedha za kumpa mchezaji na pia za klabu yake- ambayo ni dola 10,000 zaidi kutoka dola 40,000 anazotaka Kiiza.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yana SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb hakupokea simu kwa siku mbili mfululizo alizotafutwa na BIN ZUBEIRY kuzungumzia mustakabali wa Kiiza Jangwani.
  Taji la tatu Jangwani; Kiiza ameshinda mataji matatu na Yanga katika misimu yake miwili, Kombe la Kagame mara mbili na moja la Ligi Kuu Bara ambalo ndilo kainua hapa kwa kushirikiana na Simon Msuva.

  Kiiza alimaliza vizuri Mkataba wake wa kwanza wa miaka miwili Yanga SC kwa kufunga bao zuri la ushindi dhidi ya mahasimu, Simba SC miezi miwili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na wengi walitarajia hiyo ingekuwa tiketi ya kusaini Mkataba mpya, lakini sasa hali inaelekea kuwa tofauti.
  Kwa ujumla, Kiiza katika misimu yake miwili ya kuitumikia Yanga, ameiwezesha kushinda mataji matatu, mawili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na moja la Ligi Kuu Bara na ndiye aliyekuwa anaonekana mshambuliaji mwenye uhai kidogo msimu uliopita, baada ya wengine kupoteza makali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: GARI LAKWAMISHA USAJILI WA KIIZA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top