• HABARI MPYA

    Saturday, August 18, 2012

    HUYU NDIYE ZACHARIA HANS POPPE, ALIYELETWA SIMBA SC NA HAIDARI ABEID 'MUCHACHO'

    Zacharia Hans Poppe

    Na Mahmoud Zubeiry
    Hans Poppe
    MOJA kati ya mambo ambayo Simba SC iliyafaya siku za karibuni yakashitua wengi, ni usajili wa kiungo mshambuliaji, Mrisho Khalfan Ngassa kutoka Azam FC, ambaye wengi waliamini angerejea Yanga.
    Nani aliyeweza kumuweka chini na kumshawishi Ngassa akakataa ofa ya klabu yake ya zamani na kwenda kujaribu maisha mapya Msimbazi, yalipo maskani ya Simba?
    Huyo si mwingine zaidi ya Zacharia Hans Poppe, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC.
    Hans Poppe ndiye aliyefanya mazungumzo na Ngassa hadi akalainika na kukubali kupokea Sh. Milioni 12 taslimu na gari yenye thamani ya Milioni 18, sambamba na ofa ya mshahara wa Sh. Milioni 2 kwa mwezi, ambao unamfanya aendelee kuwa mchezaji mzalendo anayelipwa zaidi nchini.

    HANS POPPE NI NANI?
    Kama anavyotambulishwa, jina lake ni Zacharia Hans Poppe, ambaye alizaliwa mwaka 1956 mjini Dar es Salaam na kukulia mkoani Iringa.
    Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Zacharia alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambako alifikia cheo cha Kapteni, kabla ya kuachishwa kazi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa tuhuma za uhaini, dhidi ya serikali ya awamu ya kwanza, ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1983.
    Lakini mwaka 1995, Zacharia aliachiwa huru kwa msamaha wa rais wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, mwezi mmoja kabla hajamuachia Ikulu ya Tanzania, Benjamin William Mkapa, rais wa awamu ya tatu.
    Kama zinavyosema sheria za nchi, mtu aliyehukumiwa kifungo, hana haki ya kugombea wadhifa wowote au kuajiriwa tena, Zacharia naye hakuweza kurejea kazini, badala yake akaamua kujiajiri, kwa kuanzisha miradi yake mwenyewe, ambayo leo ikiwa ni miaka 17 baadaye, miradi hiyo imesimama imara.

    HANS POPE NA SIMBA SC:
    Alianza kuipenda Simba SC mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na zaidi mwenyewe anasema, mechi ambayo ilimfanya ajitamke rasmi yeye ni Simba damu ilikuwa dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga Juni 23, mwaka 1973, ambayo Wekundu wa Msimbazi, walishinda 1-0, bao pekee la Haidari Abeid ‘Muchacho’ dakika ya 68.
    “Nakumbuka ilikuwa ni ligi ya mtoano, tuliitoa Yanga tukaenda hadi kuchukua ubingwa kwa kuwafunga Lake kule Kigoma, kipindi kile Simba ilikuwa inaundwa na vijana wadogo wadogo tu, ilikuwa raha sana.
    Zacharia akimkabidhi jezi Daniel Akuffo

    Ngassa akisaini ofisini kwa Zacharia
    Ni Simba ambayo mwaka 1974 iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kuchukua hili Kombe ambalo linaitwa la Kagame, wakati huo linaitwa la Afrika Mashariki na Kati na pia ilifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), tukatolewa kwa fitina na Waarabu (Mehallal El Kubra),”anakumbusha Zacharia.
    Zacharia anasema aliendelea kuwa mpenzi wa Simba, hadi baadaye akaamua kuwa mwanachama.
    Lakini siku zote alikuwa pembeni, hadi lilipoundwa kundi la Friends Of Simba ndipo akaamua kujiunga nalo, ili naye aweze kutoa michango yake zaidi.
    Anasema wakati wa uongozi wa Mwenyekiti, Hassan Daalal ambao ulionekana kuelemewa na majukumu ya timu, ndipo alipata umaarufu zaidi ndani ya Simba, kutokana na kusaidia zaidi.
    Anasema uongozi wa Daalal baada ya kugundua umuhimu wake ukaamua kumpa jukumu la kusimamia fedha na anasema alifanikiwa kudhibiti fedha na kuanzisha mpango wa kuiwezesha klabu kujitegemea katika mambo mbalimbali, ikiwemo suala la usajili badala ya kutembeza bakuli.
    Anasema kutokana na kufanya vizuri katika jukumu hilo, wengi miongoni mwa wanachama na viongozi wa Simba wakamuomba agombee Uenyekiti. “Lakini siku zote kuna kitu kilikuwa kinanipa shinda. Nilikuwa sijui ni msamaha wa aina gani niliopewa na rais, unajua rais anaweza pia kutoa msamaha wa kufuta na kosa pia,”anasema.
    “Lakini nilijaribu sana kufuatilia ili kujua aina ya msamaha wangu, nilikwenda hadi Magereza, lakini hawakunipa jibu, mwishowe nikaamua kuacha tu, sasa nilipojaribu kuomba uongozi Simba, ndipo TFF wakatumia kipengele cha mimi kuwahi kufungwa kuniengua,”anasema.
    Hata hivyo, Zacharia anasema kwamba umefika wakati sheria hiyo irekebishwe kwa mtu anayetoka jela awekewe muda maalum wa kuzuiwa kushiriki katika madaraka na ajira, kabla ya kuruhusiwa kurejea kwenye maisha ya kawaida.
    “Unajua mtu anapofungwa lengo ni kumfundisha, ili baadaye akirudi uraiani awe raia mwema, sasa haiwezekani arudi uraiani halafu amewekewa vipingamizi, mimi naamini ipo haja ya kurekebisha hii sheria,”anashauri Zacharia.
    Zacharia anasema pamoja na kuukosa Uenyekiti, anashukuru amepata fursa ya kuendelea kuisaidia klabu yake, baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili.
    “Nimesaidia sana kuiwezesha klabu kukusanya fedha na kutunza, ambazo zimetuwezesha kujitegemea kufanya usajili wetu kwa takriban asilimia 85.  Na ni fedha ambazo zimetokana na mapato ya milangoni, udhamini wa TBL, pango za majengo ya klabu na mauzo ya wachezaji (Mbwana Samatta, Patrick Ochan na Mussa Mgosi) na nyingine kutokana na michango tunayojichangisha,”anasema.

    NINI JUKUMU LA KAMATI YA USAJILI YA SIMBA?
    Hans Poppe
    Zacharia anasema kwamba, Kamati yake hupokea mapendekezo kutoka kwa Kamati ya Ufundi juu ya aina ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa, ndipo wao hutafuta wachezaji.
    “Kwanza, Kamati ya Ufundi inakuwa imekutana na benchi la ufundi, imepewa ripoti ya kitaalamu, wanajadiliana ndio wanatuletea orodha ya wachezaji wanaotakiwa kwa maana ya nafasi zao. Sasa sisi tunakwenda kufanya tathmini ya wachezaji gani bora ndani na nje ya nchi, tukiwapata, tunarudi kwa Kamati ya Ufundi, tunawapa majina, sasa wao ndio wanakwenda kuwafuatilia uwezo wao na wakiridhika, wanatupa jibu, sisi ndio tunawasaini,”anasema.
    Akifafanua, Zacharia anasema kwamba hakuna mtu anayesajili kwa fedha zake Simba SC, bali ni fedha za klabu.
    “Sisi Kamati ya Usajili tunapotaka kumsajili mchezaji, tunakwenda kwa Kamati ya Fedha, sasa wao ndio wanatuambia uwezo wao unafikia wapi, pale ambako pamezidi sasa tunatoka tunakwenda kuchangishana na ndugu zetu Friends Of Simba na wadau wengine tunamalizana na mchezaji,”anasema.
    Anasema ndani ya Simba SC hivi sasa hakuna utaratibu wa mtu mmoja kumsajili mchezaji kwa fedha zake, kwa sababu hiyo imewahi kuleta matatizo ndani ya klabu miaka ya nyuma na sasa wamechukua tahadhari.
    “Inatokea mtu anatofautiana na uongozi, anaamua kumtumia mchezaji wake kuihujumu timu, sasa hiyo haipo tena,”anasema.
    Alipoulizwa kuhusu wachezaji kusajiliwa na kuachwa kabla hawajaitumikia timu, Zacharia anasema; “Hao ni wale ambao wanaingia nje ya utaratibu tuliojiwekea, inatokea mtu tu anaamua kumsajili kwa utashi wake na fedha zake. Na ikitokea hafai sisi tunamkata tu. Ila inatokea mtu anasajili mchezaji, anamleta, tunamuona anafaa, tunampitisha, ila lazima apite katika utaratibu wetu tuliojiweka na anasaini mkataba na klabu, si mtu,”anasema.
    Lakini Zacharia anasema kwamba kutokana na kiwango cha mishahara kutoka kwa wadhamini wao wakuu, TBL (kupitia Kilimanjaro Premium Lager)- inabidi baadhi ya wachezaji ambao wanalipwa zaidi, fedha zitoke nje ya utaratibu wa kawaida. Ndiyo utaona mtu katika mkataba wake analipwa kiasi fulani, lakini kiasi kingine kipo katika makubaliano mengine,”anasema.
    Lakini Zacharia anasema kutokana na mradi wao wa timu za vijana kuendelea vizuri, anaamini itafika wakati Simba SC haitakuwa ikitumia fedha nyingi katika kusajili na pia itakuwa ikiingiza fedha nyingi katika kuuza wachezaji.
    “Tuna timu nzuri ya U-17 na U-20 na kama uliona U-20 imeitoa timu ya wakubwa ya Azam FC katika michuano ya Bank ABC na Jumamosi inacheza fainali na Mtibwa Sugar tukiwa na matumaini makubwa ya kuchukua Kombe, wachezaji wote wa timu za vijana wanalipwa mishahara, makocha wao wanalipwa pia, kwa ujumla timu zinahudumiwa vizuri na tumepata wachezaji wasiopungua watano wa kupandisha kikosi cha kwanza msimu huu.
    Wengine wapo hadi timu ya taifa ya wakubwa, kama yule kijana Messi (Ramadhani Singano) na Mkude (Jonas Gerald). Na tayari kuna wachezaji wa timu ya vijana ya Simba wana ofa ya kwenda kufanya majaribio Ulaya, kwa hivyo unaweza kuona tunaelekea kuzuri,”anasema.

    NINI DUKUDUKU LAKE?
    Vurugu katika usajili na uendeshaji soka kwa ujumla, ni vitu ambavyo Zacharia hataki hata kuvisikia. Anatolea mfano Yanga walivyofanya kwa beki wa APR ya Rwanda, Mbuyu Twite, kwamba hayo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati.
    “Mwenzako amekwishazungumza na mchezaji, wewe huna sababu ya kwenda kuzungumza naye na kumrubuni, kupandisha dau, hayo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati.
    Tazama kwa mfano usajili wa Robin van Persrie kutoka Arsenal, Manchester United wamemalizana naye kistaarabu, japokuwa Manchester City nao walikuwa wanamtaka, lakini hukuwasikia kumfuata mchezaji eti kuahidi kumpandia dau, huo sio ustaarabu, mwenzako akishamalizana na mchezaji, wewe tafuta mwingine.
    Ona sisi Simba, Yanga wametupokonya Kevin Yondan, tumemfuata Twite, wamemchukua pia, lakini bado tumepata beki mwingine mzuri tu, tena zaidi ya hao wote, hakuna haja ya kugombea mchezaji,”anasema, Zacharia, baba watoto wa tisa, kutoka kwa mama wanne tofauti.    
    Mahojiano kati ya BIN ZUBEIRY na Zacharia Hans Poppe yalifungwa kwa swali kuhusu timu anazopenda na wachezaji kwa sasa duniani, ambalo majibu yake ni; “Ulaya napenda Arsenal pale England, Bayern Munich pale Ujerumani na Barcelona kwa Hispania… kwa wachezaji kwa kweli ni Alex Song, Robin van Persie na Frank Ribbery,”.
    Hans Poppe akimkabidhi jezi Paschal Ochieng

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUYU NDIYE ZACHARIA HANS POPPE, ALIYELETWA SIMBA SC NA HAIDARI ABEID 'MUCHACHO' Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top